TANAPA yashinda tuzo kwa utoaji wa huduma za uhifadhi na utalii




Shirika la hifadhi za taifa Tanzania TANAPA limesema kwamba limeshinda tuzo ya kuwa shirika bora duniani kwa utoaji wa huduma za uhifadhi na utalii.


Kulingana na TANAPA, tuzo hiyo imetolewa na taasisi ya utafiti ya kimataifa ya nchini Uswis, na kwamba nchi 39 kote duniani zilikuwa zinashindania tuzo huyo.



Katika makao makuu ya shirika hilo yaliyopo Arusha kaskazini mwa Tanzania, msemaji wa TANAPA Pascal Shelutete, amewaambia waandishi wa habari kwamba tuzo hiyo imeiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizo na mashirika bora kabisa duniani yanayohusika na masuala ya utalii na uhifadhi. Ushindi huo unahusisha mashirika mengine 51 kutoka nchi 39 zilizokuwa zikishindania tuzo hiyo. 



Shelutete amesema: “Na uteuzi huu wa shirika la hifadhi Tanzania kuwa mshindi wa tuzo hizi, umetolewa na taasisi ya nchini Uswis inayofahamika kama European Society for quality research ESQR wa viwango kwa wateja wake kwahiyo TANAPA kwa mwaka 2020, imeteuliwa kuwa mshindi kidunia”. 



Shirika hilo la Uswisi hutoa tuzo hiyo kila mwaka kwa kuhusisha taasisi za serikali na zisizo za serikali kote duniani, ambazo zinatoa huduma  viwango vya juu katika masuala ya uhifadhi na utalii.



Tanzania kupitia hifadhi za taifa TANAPA, imepata tuzo ya kiwango cha dhahabu ambacho ni kiwango cha juu kabisa cha ushindi duniani. Washindi wa tuzo hiyo huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.



TANAPA:Tuzo hiyo inaiweka Tanzania katika ramani nzuri ya kutangaza biashara ya utalii



TANAPA inasema tuzo hii, inaiweka Tanzania katika ramani nzuri ya kutangaza biashara ya utalii, ambayo hata hivyo imeporokomoka vibaya kutokana na janga la Corona.



Tanzania ina lengo la kufikisha watalii milioni tano kwa mwaka kutoka watalii milioni moja na nusu mpaka milioni mbili wanaoitembelea nchi hiyo kwa sasa kutoka mataifa mbalimbali kama anavyofafanua zaidi Pascal Shelutete.



“Inaendana sambamba kabisa na malengo ya kitaifa ambayo yanatutaka sisi wote ambao tunahusika na sekta ya utalii, kufikisha lengo la watalii milioni tano itakapofika mwaka 2025.” 



Hata hivyo ushauri unatolewa kwa Tanzania, kuendelea kuimarisha biashara ya utalii, na watanzania wanufaike nao kwani wengi wao ndio wanaozilinda hifadhi hizo za taifa. Joseph Mwenda ni mtaalamu wa mazingira.



“Ni wakati sasa Tanzania kuweza kuweka nguvu kubwa zaidi katika kuhifadhi ikolojia ya viumbe mbali mbali. Ninapozungumzia suala la ikolojia ninamaanisha ikolojia ya mimea na ikolojia za viumbe ambavyo vinaishi nadani ya uoto ulio kwenye hifadhi.” 



Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Jestas Nyamanga, ataipokea tuzo hiyo juma lijalo mjini Brussels Ubelgiji kwa niaba ya TANAPA.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad