Katika hatua nyengine, Rais Trump ameonya kwamba ataibebesha lawama Iran, endapo raia wa Marekani walioko nchini Iraq watashambuliwa, katika wakati ambapo kumbukumbu ya kwanza ya mauaji dhidi ya kamanda wa juu wa jeshi la Iran ikikaribia.
Kupitia ujumbe wake wa Twitter, Trump ameandika kwamba ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ulishambuliwa kwa makombora kadhaa siku ya Jumapili, ambayo amedai kuwa yalitokea Iran. Kupitia ujumbe huo, amesema kwamba endapo Mmarekani mmoja tu atauawa, ataiwajibisha Iran.
Waziri wake wa mambo ya kigeni, Mike Pompeo, tayari alishainyooshea kidole cha tuhuma Iran, huku kamandi ya kijeshi kwenye eneo la Ghuba ikisema kuwa mashambulizi hayo ya maroketi yalifanywa na kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Mnamo tarehe 3 Januari mwaka huu, Trump aliamuru mashambulizi ya anga dhidi ya kamanda wa juu wa jeshi la Iran, Kassim Suleimani, aliyekuwa ziarani mjini Baghdad.