Hukumu ya kifo ya mfungwa Brandon Bernard imetekelezwa jimboni Indiana baada ya ombi la dakika za mwisho kutenguliwa kwa hukumu kukataliwa na Mahakama kuu ya Marekani
Bernard mwenye miaka 40, alihukumiwa kwa makosa ya mauaji mwaka 1999 alipokuwa kijana mdogo, na alikuwa mhalifu mdogo kuhukumiwa na serikali katika kipindi cha miaka karibu 70.
Bernard aliiambia familia ya wenza aliowaua kuwa anaomba msamaha, kabla ya kuuawa kwa kuchomwa sindano siku ya Alhamisi.
Hukumu nyingine nne za vifo zimepangwa kutekelezwa kabla Donald Trump hajaondoka madarakani.
Ikiwa yote matano yatafanyika, Bwana Trump atakuwa amesimamia hukumu zaidi za kifo katika kipindi cha zaidi ya karne moja. Na kufanya idadi yake kufikia 13 tangu mwezi Julai.
Bernard alitangazwa kuwa amekufa saa 21:27 za huko siku ya Alhamisi sawa na saa 11 siku ya Ijumaa katika gereza la jela la Terre Haute.
Kabla ya hayo alielekeza maneno yake ya mwisho kwa familia ya walioathirika, akizungumza kwa utulivu kwa zaidi ya dakika tatu.
''Ninaomba radhi. Haya ni maneno pekee ninayoweza kusema kuelezea namna ninavyojisikia sasa na namna nilivyojisikia siku hiyo,'' alisema, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press.
Utekelezaji wa hukumu ya kuuawa ulicheleweshwa kwa zaidi ya saa mbili baada ya mawakili wa Bernard kuitaka Mahakama kuu kusitisha- lakini ombi hilo lilikataliwa.
Bernard alipewa adhabu ya kifo kwa kuhusika kwake katika mauaji ya Todd na Stacie Bagley mnamo Juni 1999.
Alikuwa mmoja wa vijana watano wanaotuhumiwa kuwaibia wawili hao na kuwalazimisha kuketi nyuma ya gari lao huko Texas.
Walipigwa risasi kwenye gari na mwenzao wa miaka 19 Christopher Vialva kabla ya Bernard kulichoma moto gari.
Mchunguzi huru aliyeajiriwa na upande wa utetezi alisema Stacie alikuwa amekufa kabla ya moto.
Walakini, ushuhuda wa serikali wakati wa kesi hiyo ulidai kwamba ingawa Todd Bagley alikufa papo hapo, Stacie alikuwa na masizi katika njia yake ya hewa, akiashiria kwamba alikufa kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na sio jeraha la risasi.