Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Bi. Nuru Mhando pamoja na Meneja wa matumizi ya fedha wa TPA, Bi. Witness Mahela ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.
Majaliwa amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika hesabu ya Bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019 lengo la ukaguzi huo lilikuwa kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma ambapo ripoti hiyo ilidhihirisha ubovu katika Bandari ya Kigoma.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Mashitaka (DCI), Robert Boaz ahakikishe mfanyabiashara wa duka la ujenzi mjini Kigoma Bw. Eliya Mtinyako na Mhasibu wa Bandari ya Kigoma Madaraka Madaraka wanatafutwa popote walipo na kukamatwa, nakuagiza watumishi wote waliosimamishwa kazi wachunguzwe haraka na ikibainika kwamba hawana hatia warejeshwe kazini na wakikutwa na hatia hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye kikao na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Menejimenti ya Mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DCI) leo jijini Dar es salaam.
Amesema katika hali isiyokuwa ya kawaida TPA iliidhinisha malipo ya sh. bilioni 8.2 kwenda Bandari ya Kigoma kwa ajili ya kwenda kufanya malipo mbalimbali huku ukomo wa bandari hiyo ni sh. bilioni 7.4, fedha hizo zilitumika kufanya malipo yasiyostahili kwa watu mbalimbali akiwemo mfanyabiashara wa duka la ujenzi mjini Kigoma Bw. Eliya Mtinyako aliyelipwa zaidi ya shilingi milioni 900 huku mhasibu wa bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka alifuta madeni ya zaidi ya shilingi bilioni moja waliyokuwa wakidaiwa wateja bila ya kufuata taratibu na kuisababishia Serikali hasara.
Aidha Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa TAKUKURU afanye uchunguzi kuhusu Bw. Kalibilo ambaye ameonekana kuingiziwa kiasi kingi cha fedha bila ya kuwepo nyaraka zinazoonesha sababu za mtumishi huyo kulipwa fedha hizo.
“Agosti anaonekana alilipwa shilingi milioni 55, Septemba shilingi milioni 53, Oktoba shilingi milioni 37 na Novemba shilingi milioni 19, lazima atafutwe popote alipo ijulikane fedha hizo alilipwa kwa ajili gani.” amesema Waziri Majaliwa