Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amemuagiza mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula kuwabaini wanaohujumu visima vya maji kwa kujaza mawe.
Agizo hilo amelitoa baada ya Meneja wa Wakala wa Usambazaji wa Maji na usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Manyara Mhandisi Walter Kirita, kueleza kuwa miradi ya maji katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya Simanjiro inachelewa kukamilika kutokana na watu walio na nia ovu kuharibu miundombinu ya visima vya maji kwa kujaza mawe.
Akizungumza katika kikao cha thelathini cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika leo desemba 22,2020, Mkuu wa mkoa amesema hakuna hujuma yoyote inayokubalika hivyo wahusika wachukuliwe hatua za kisheria haraka.
Mkirikiti amesema watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yanayofanyiwa hujuma, lazima wawajibike kwa kuwa zinazopotea ni pesa za walipa kodi.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula amesema watafanya jitihada kuwabaini wahusika na kuwashtaki kwa kosa la uhujumu Uchumi.
Awali mbunge wa jimbo la Simanjiro Christiopher Ole Sendeka alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika kijiji cha Olchoronyori sio ya kuridhisha kwani wananchi wa eneo hilo wanafuata huduma ya maji umbali wa kilomita thelathini.