Jopo la waatalamu nchini Marekani limeidhinisha matumizi ya dharura ya chanjo ya virusi vya corana iliyotengenezwa na kampuni za Pfizer na BioNTech uamuzi unaoruhusu kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo kwa umma wa Marekani.
Wataalamu 17 kati ya 22 walioteuliwa na mamlaka ya dawa na chakula ya Marekani walipiga kura za ndiyo kuidhinisha matumizi ya chanjo hiyo ambayo itatolewa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 16 na kuendelea.
Uamuzi huo umekuja wakati Marekani, taifa lililoathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona jana lilirikodi vifo vya watu 3,000 na kuifanya idadi ya waliokufa kutokana na COVID-19 kukaribia watu 300,000.
Marekani inalenga kuwachanja watu milioni 20 mwezi Disemba huku wafanyakazi wa afya na watoa huduma za msaada wakiwa kwenye orodha ya kwanza ya wale watakaopatiwa chanjo.