Watu 9 wamefariki dunia leo baada ya moto kuzuka kwenye jengo la wagonjwa mahututi wa COVID-19 katika hospitali moja ya binafsi kusini mwa Uturuki.
Kulingana na waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca chanzo cha moto huo ni kuripuka kwa mtungi wa gesi ya Oksijeni. Shirika la Habari la Uturuki, Anadolu, limeripoti kuwa moto huo umetokea kwenye hospitali ya chuo kikuu cha Sanko iliyopo kilometa 850 kusini mashariki ya mji wa Instabul.
Taarifa ya Hospitali hiyo imesema moto uliozuka ulidhibitiwa haraka na kuongeza kuwa watu waliokufa ni wenye umri wa kati ya miaka 56 na 85 Sehemu kubwa ya vyumba vya wagonjwa mahututi nchini Uturuki vina idadi kubwa ya wagonjwa inayopindukia asilimia 74 kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.