WASHTAKIWA wote wanne katika shauri namba tisa la mauaji ya kukusudia ya Alphonce Mawazo aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrais na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa wamekana kuhusika kwenye tukio hilo huku baadhi wakidai mashtaka dhidi yao ni ya kutengenezwa.
Ushahidi wa washtakiwa hao ulioanza kutolewa juzi saa tisa alasiri katika mahakama kuu Kanda ya Mwanza iliyoketi katika mahakama ya hakimu mkazi Geita umekamilika jana Jumanne Desemba 15, 2020 saa 7 mchana.
Mshtakiwa wa kwanza, Alfan Apolnar, amekana mashtaka yote na ushahidi dhidi yake akidai siku ya tukio alikuwa mgonjwa na alikuwa amelazwa katika zahanati ya Segese iliyopo wilaya ya Kahama.
Ameiomba mahakama itende haki kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ni wa kutengeneza kwa sababu shahidi namba tisa Said Omary aliyemtaja kuhusika, maelezo yake yamejichanganya baada ya kudai alikuwa amebeba mteja kupeleka ofisi za CCM lakini akiwa mahakamani alidai kuwa yeye ndio aliyekuwa amempakia Mawazo.
Amedai pia shahidi huyo namba tisa aliieleza mahakama kuwa sasa ana miaka 20 na ameanza kuendesha bodaboda tangu mwaka 2004 na kujichanganya kusema 2006 jambo ambalo linaonyesha maelezo hayo ni ya kutengeneza.
Maelezo kama hayo yametolewa na mshtakiwa wa pili, Epafra Zakaria aliyesema siku ya tukio alikuwa kwenye semina ya uchaguzi mdogo wa udiwani Katoro na kwamba shahidi namba tisa katika kesi hiyo alieleza kuwa yeye ni mkodisha baiskeli jambo ambalo ni uongo na kwamba yeye ni mfanyabiashara mkubwa.
Mstakiwa namba tatu, Hashim Sharif ameomba mahakama kumuachia huru kwa kuwa hajahusika na mauaji hayo na kwamba ushahidi uliotolewa na shahidi namba nne na tisa dhidi yake siyo wa kweli.
Ameileza mahakama kuwa mashahidi hao wamedai mahakamani kuwa yeye ni mchezaji wa mpira wa timu ya Katoro Star jambo ambalo sio kweli kwa kuwa wakati anakamatwa alikuwa na umri wa miaka 45.
Mshtakiwa wa tano ni Kalulinda Bwire amedai siku ya tukio alikuwa kwenye semina ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Ludete na alikamatwa Novemba 16, 2015 baada ya kuwa wakala kituo cha stoo namba mbili kilichopo kata ya Ludete.
Bwire pamoja na kukabidhi kielelezo cha fomu namba sita ya kiapo cha kutunza siri za uchaguzi, ameomba mahakama kumuachia huru kwa kuwa hahusiki na mauaji hayo.