Vikosi vya usalama vimewaokoa karibu wanafunzi 350 wa kiume waliotekwa nyara na wanamgambo wa itikadi kali kaskazini mwa Nigeria na kupelekwa msituni. Walichukuliwa mateka shuleni Kankara siku sita zilizopita
Gavana wa jimbo la Katsina Aminu Bello Masari amesema jumla ya wavulana 344 waliokuwa wanashikiliwa katika Msitu wa Rugu katika jimbo jirani la Zamfara wameachiliwa huru.
Katika tangazo alilofanya kwenye televisheni ya taifa NTA jana usiku, gavana huyo amesema wavulana hao wamepelekwa katika jimbo la Katsina kufanyiwa uchunguzi wa matibabu na kukabidhiwa kwa familia zao. Hakufichua kama serikali ilitoa kikomboleo chochote.
Katika operesheni hiyo ya uokozi, vikosi vya usalama vililizingira eneo ambalo vijana hao walikuwa wanashikiliwa na vilikuwa vimepewa maagizo ya kutofyatua risasi hata moja.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amepongeza kuwachiwa kwao, akisema ni ahueni kubwa kwa familia zao na nchi nzima na kwa jamii ya kimataifa.
Wakati kukiwa na kilio katika taifa hilo la Afrika Magharibi kuhusu ukosefu wa usalama kaskazini mwa nchi, Buhari alibainisha juhudi zilizofanikiwa za serikali yake kuhakikisha kuwachiwa kwa wanafunzi waliochukuliwa mateka siku za nyuma. Amekiri kuwa eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ni changamoto kubwa ambayo utawala wake umedhamiria kukabiliana nayo.
Kundi la Boko Haram chini ya kiongozi wake Abubakar Shekau lilidai kuhusika na utekaji nyara huo wa Ijumaa wiki iliyopita katika shule moja ya sekondari ya serikali katika mji wa Kankara, jimboni Katsina.
Zaidi ya wanafunzi 800 walikuwa shuleni wakati wa shambulizi hilo. Mamia walitoroka lakini inaaminika Zaidi ya 330 walichukuliwa mateka.
Kwa Zaidi ya miaka kumi, Boko Haram imekuwa ikiendesha harakati za umwagaji damu kwa lengo la kuanzisha sheria kali za kiislamu kaskazini mwa Nigeria.
Maelfu ya watu wameuawa na Zaidi ya milioni moja wameachwa bila makazi kufuatia machafuko hayo.
Jimbo la Katsina lilifunga shule zake zote za mabweni ili kuzuia utekaji nyara mwingine. Majimbo jirani ya Zamfara, Jigiwa na Kani pia yamefunga shule zao kama tahadhari.
Mnamo Februari 2014, wavulana 59 waliuawa wakati wanamgambo walipovamia chuo cha serikali kuu cha Buni Yadi katika jimbo la Yobe. Aprili 2014, Boko Haram ikawateka nyara wasichana 270 kutoka shule ya bweni ya serikali mjini Chibok jimbo la kaskazini mashariki la Borno. Karibu 100 kati yao bado hawajulikani waliko.
Mwaka wa 2018, Boko Haram waliwarejesha katibu wasichana wote 110 waliokuwa wamewateka kutoka shule moja ya bweni katika mji wa Dapchi.