Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mji wa Geita Bw. Modest Joseph Apolinary kupisha uchunguzi kufuatia ununuzi wa gari yenye dhamani shilingi millioni 400
Akiongea leo na Menejimenti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI Jijini Dodoma Waziri Jafo amesema kuwa mara baada ya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baraza la Madiwani kuvunjwa majukumu yote yalikasimishwa kwa wakurugenzi na kupelekea baadhi ya Halmashauri kutumia muanya huo kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
“Halmashauri ya Mji wa Geita katika kipindi hicho ambacho baraza la madiwani halipo waliweza kununua gari lenye dhamani ya shilingi milioni 400, jambo hili halikubaliki kwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma”amesisitiza Waziri Jafo
Ameendelea kufafanua kuwa Geita wanafursa nyingi ya madini lakini wamenunua gari moja kwa gharama hiyo wakati katika eneo hilo kunauhitaji mkubwa wa vituo vya afya, madawati na vyumba vya madarasa, jambo hili ni kinyume na maadili ya kiutumishi na linarudisha nyuma juhudi za Serikali za kutoa huduma bora kwa wananchi
Waziri Jafo amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga kuunda timu ya uchunguzi ambayo itachunguza kwa kina matumizi ya fedha katika Halmashauri ya Mji Geita
Pia amemuagiza katibu Mkuu huyo kufanya uchunguzi zaidi kwa mwanasheria na mwekahazina wa Halmashauri hiyo wakiwa ni washauri wakuu wa Mkurugenzi ni kwa jinsi gani waliweza kutimiza majukumu yao kikamilifu katika kushauri kuhusu ununuzi wa gari hilo.
Sambamba na hilo Waziri Jafo amekiagiza Kitengo cha ukaguzi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kufanya uchunguzi na ufuatiliaji kwa Halmashauri nyingine zenye kutiliwa shaka kama zilienda kinyume cha taratibu ya matumizi ya fedha.
Aidha,amemuagiza Katibu Mkuu kuunda timu itakayochunguza Ofisi ya Mkurugenzi, Manunuzi, Mwekahazina na Wakuu wa vitengo wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda juu ya tuhuma zinazotolewa na wananchi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika Halmashauri hiyo, ili endapoitabainika kuwa ni kweli hatua sitahiki zitachukuliwa kwa wahusika.