Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kanda ya Pasifiki Magharibi Dk. Takeshi Kasai, ameonya kuwa chanjo ya corona (Covid-19) haitamaliza janga hilo kwa muda mfupi, na nchi za Pasifiki Magharibi zinaweza kuwa na shida na upatikanaji wa chanjo mapema.
Kulingana na taarifa iliyoandikwa na gazeti la South China Morning Post, Kasai alisema kwamba uanzilishi wa chanjo kwa wingi katika nchi za Pasifiki Magharibi unaweza kufikia katikati ya 2021.
Alisema, "Chanjo sio kitu cha rahisi kinachoweza kumaliza janga hilo kwa haraka."
Takeshi alisisitiza kuwa nchi zinaweza kupata chanjo kwa kiwango dogo mwanzoni, kwa hivyo wale walio walio na hali hatari zaidi ya kiafya ndio wanapaswa kupewa kipaumbele.
Aliongezea kusema, "Ikiwa tunaweza kuwekeza kwa kiwango kizuri ili kutoa chanjo, tunaweza kuwa na chanjo za kutosha kwa ajili ya watu wanaopewa kipaumbele katika nchi zote ifikapo mwisho wa 2021. Kwa wale wengine wasiokuwa na hali ya hatari kubwa, inaweza kuchukua miezi 12 hadi 24. Hata hivyo, hali zisizo na uhakika na zisizotabirika zinaweza kutokea."
Takeshi pia alifananisha chanjo na taa iliyo mwisho mwa handaki kwa kusema,
"Ingawa tumechoka sasa, lazima tuendelee kuchukua hatua za kujilinda sisi wenyewe binafsi pamoja na wale wanaotuzunguka kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kuzingatia umbali wa masafa wa kijamii na kuepuka maeneo yenye hatari kubwa ."
WHO inawatambua watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi na wafanyikazi wa huduma ya afya wanaopambana na Covid-19 kama kikundi cha "hatari", na inapendekeza kwamba wapewe kipaumbele kwa chanjo.