Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha dhidi ya wasiwasi wa kupindukia kuhusu aina mpya ya virusi vya corona vinavyosambaa kwa kasi kubwa, baada ya kugunduliwa nchini Uingereza na baadae Afrika Kusini.
WHO imesema ni kawaida ya virusi kufanya hivyo wakati wa janga, baada ya aina hiyo ya virusi kuzua taharuki kote ulimwenguni, hali iliyopelekea mataifa kadhaa kuweka vizuizi vya usafiri kwa Uingereza na Afrika Kusini.
Maafisa wa WHO wamesema hawana ushahidi wowote unaoonyesha kwamba aina hiyo mpya ya virusi inawafanya watu kuwa wagonjwa zaidi au kuwa ni mbaya zaidi kuliko virusi vilivyokuwepo awali vya ugonjwa wa COVID-19. Ingawa WHO imethibitisha kwamba aina hiyo mpya inaonekana kuenea kwa kasi zaidi.