Akamatwa Austria na vinyonga 74 kutoka Tanzania





Vinyonga 74 wameokolewa na kupelekwa kwenye bustani ya wanyama ya nchini Austria baada ya kubainika wakiwa kwenye sanduku katika uwanja wa ndege wa Vienna.
Wanyama hao waligunduliwa na maafisa wa usalama baada ya picha ya ukaguzi ya X-Ray ya sanduku kutiliwa shaka. Vinyonga 74 walikutwa wamefichwa kwenye soksi na mikebe.

Viumbe hao wangeuzwa kwa gharama ya dola za Marekani 44,970 kwenye soko haramu, maafisa wamesema. Mwanaume huyo mwenye miaka 56 aliyesafiri kutoka Tanzania alikamatwa baadaye.

Mtu huyo anaweza kutozwa faini ya mpaka kiasi cha Euro 6,000, Wizara ya Fedha imeeleza. ''Vinyonga wanaweza kujificha vizuri...lakini hawakufua dafu mbele ya picha za ukaguzi,'' Wizara ilisema katika taarifa yake.

Wanyama baadaye walisafirishwa kwenda kwenye bustani ya wanyama ya Vienna, Schönbrunn , ambako walifanyiwa uchunguzi na wataalamu.

Vinyonga watatu hawakumudu safari.

Umri wa vinyonga hao wana umri wa kuanzia wiki moja na zaidi.

''Kwa mujibu wa wataalamu kwenye bustani hiyo, viumbe hao wanatoka kwenye milima ya Usambara, eneo la mazingira ya baridi,'' Wizara ya fedha imeeleza.

Vinyonga walio hai wanatunzwa katika bustani ya Schönbrunn.

Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania Allan Kijazi akizungumza na Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania amesema wanazo taarifa kuhusu tukio hilo na kuwa wanafuatilia suala hilo.

Akinukuliwa na gazeti hilo amesema ''mchezo mchafu '' umefanyika.

Amesema wanafuatilia kujua ni namna gani mtu huyo alipita katika viwanja vya ndege bila kukamatwa

''Tumewasiliana na wenzetu wa interpol ili wafuatilie, wahusika warudishwa nchini, wachukuliwe hatua na hao vinyonga warudishwe.'' Alilieleza Mwananchi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad