Aliyedaiwa kumnasa vibao mjamzito akutwa na hatia






Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemkuta na hatia Muuguzi Valentine  Kinyanga wa kituo cha afya Mazwi ambaye alilalamikiwa kwa kosa la kumpiga vibao mama aliyefika kujifungua kituoni hapo mnamo tarehe 5 Januari, mwaka huu.


Akisoma hukumu hiyo jana mbele ya wakili wa Serikali Fortunatus Mwandu, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania  Abner Mathube alisema kuwa Baraza limemtia hatiani mlalalamikiwa chini ya kifungu 26(a)(c) ya sheria ya uuguzi na ukunga kwa kosa la kwanza na la pili.



Mathube alisema kuwa baraza lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa kinyume na kifungu 25(3)(c)cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania.



Katika kosa la kwanza  lililotolewa ushahidi ulithibitisha kuwa ni kweli  mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa alikiri kumpiga mlalamikaji



Aidha, kosa la pili lilikuwa ni kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma kinyume na kifungu 25(3)(k) lilithibitika kwa mtuhumiwa  kushindwa kufuata utaratibu wa utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji, kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutolea huduma na kuruhusu mtu  ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji(mgonjwa)



“Kwa kuzingatia utetezi wa mlalamikiwa na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji na mashahidi, umethibitisha  mashitaka yote kama alivyo shatakiwa na mlalamikaji na kwa kuangalia uzito wa makosa yaliyobainishwa dhidi ya mlalamikaji ya kwamba  angeweza kusababisha madhara makubwa kwa kumchapa vibao mama ambaye alikua tayari amejifungua pasipo msaada wake,Muuguzi huyo alipaswa kumuhudumia kwa kwa weledi na upendo mkubwa”.



Aliongeza kuwa kutokana na hayo Baraza limempa adhabu ya kumuondoa kwenye orodha (Rolls) ya wauguzi na wakunga Tanzania chini ya kifungu 28(3)(a) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ya mwaka 2010 na kutakiwa kurejesha vyeti na leseni  kwa muuguzi mkuu  wa mkoa wa Rukwa ambaye atawasilisha kwa Baraza.



Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema  haki ya rufaa imeelezwa chini  ya kifungu 31(1) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ambapo anaweza kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya hukumu.



Mara baada ya hukumu hiyo kutolewa  Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluya amewata wauguzi kufanya kazi kwa weledi licha ya changamoto ya watumishi hasa katika kada ya uuguzi.



Baluya amewataka wauguzi wote nchini  kuishi kwa kufuata miongozo ya taaluma yao kwani kukiuka maadili ya taaluma yao inawaondolea sifa na kuonekana muuguzi sio rafiki wa mteja.



Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi Baluya alisema suala hili lipo mamlaka nyingine hivyo wauguzi  wanapaswa kulinda hadhi ya taaluma yao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mahali walipo.



Mnamo tarehe 5 Januari,2021 saa nne usiku, ilidaiwa Muuguzi Valentine Kinyanga alimpiga vibao Zulfa Said ambaye alifika kituo cha afya Mazwi kujifungua na hivyo Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania kuamua kufuatilia tuhuma hizo  na hatimaye kumkuta na hatia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad