Kanisa la Kianglikana nchini Uganda limemvua cheo aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa hilo, Stanley Ntagali, na kusitisha utendaji wa majukumu ya uaskofu pamoja na kuzuiwa kuwakilisha kanisa hilo kabisa kwasababu ya madai ya uzinzi.
Bwana Ntagali alistaafu mwaka jana Machi baada ya kuhudumu kwa miaka 43 kama askofu.
Katika taarifa ya Januari 13 kwenye tovuti ya kanisa la Kianglikana mrithi wake Dkt. Stephen Samuel Kaziimba, amesema Bwana Ntagali alijihusisha na mahusiano na mwanamke mmoja aliyekuwa kwenye ndoa na hilo alilifahamu.
"Alisaliti ofisi ya Askofu, kiapo alichokula wakati wa kuapishwa, na maadili mema aliyotekeleza kwa kujitolea," Dkt. Kaziimba ameongeza.
Dkt. Kaziimba amesema kanisa la Uganda limejitolea kuwa na uwazi pamoja na kutoa uangalinzi wa uchungaji kwa wale ambao wameathirika na hali hiyo na kutoa wito wa maombi kwa wanandoa wote, kuomba msahama na maridhiano.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Amerika Kaskazini, Foley Beach, pia naye alitoa taarifa yake akionesha kusikitishwa na tukio hilo.
"Stanley ni ndugu katika Yesu ambaye nimekuwa nikifurahia kufanya kazi naye kwa miaka mingi na inanisikitisha sana kusikia mambo hayo. Ni maombi yangu mbele ya Mungu kuwa ataendelea na njia ya kuomba msamaha na kwamba Mungu atafariji wote walioathirika na dhambi hii."
Stanley Ntagali, aliyekuwa Askofu hakupatikana kutoa maoni yake kuhusiana na kusimamishwa uaskofu.
Lakini raia wengi wa Uganda watamkumbuka kwa kuzungumzia kile ambacho alikiona kama maadili mabaya nchini humo, 2019 aliyenukuliwa na gazeti la eneo akishauri watu “kudhibiti matamanio yao ya kingono”.
Kanisa la Kianglikana nchini Uganda limekadiriwa kuwa na wafuasi milioni 13.