MWITA Buruna (30), mkazi wa kijiji cha Rung’abure Wilaya ya Serengeti mkoani Mara amelazwa hospitalini baada ya kuchomwa kisu tumboni katika ugomvi wa kugombea Sh1,000.
Akisimulia tukio hilo lililotokea Januari 15, 2021, mwenyekiti wa kijiji cha Rung’abure, Joseph Meng’anyi, amesema ugomvi kati ya wawili hao ulitokana na kupotea kwa simu ya kiganjani ya Buruna wakati wakinywa pombe za kienyeji katika moja ya vilabu vinavyouza pombe za kienyeji kijijini hapo.
“Ugomvi huo ulitokea baada ya Buruna kugundua kupotea kwa Sh1,000 aliyoificha ndani ya mfuniko wa simu ndipo akamtaka Bisako kumrejeshea fedha yake bila mafanikio,” amesema Meng’anyi.
Kutokana na Bisako kugoma kumrejeshea fedha yake, Burana aliamua kuchomoa kadi ya miziki aliyokuwa anatumia Bisako kupigia muziki na hivyo kuibua malalamiko kutoka kwa wateja kutokana na burudani kukatika.
“Baada ya mzozo wa muda mrefu, Bisako alirejesha Sh1,000 aliyoichomoa kutoka kwenye mfuniko wa simu ya Buruna huku wawili hao wakianza kutoleana maneno makali kabla ya kusukumana nje walikoendelea na ugomvi,” amesema Meng’anyi.
Amebainisha kuwa katika ugomvi huo, Burana alichomoa kisu kidogo alichokuwa nacho bila kujua mwenzake alikuwa na kisu kikubwa zaidi ambacho alikitumia kumjeruhi na kutokomea kusikojulikana hadi sasa. Mganga Mkuu wa Hospitali teule ya Nyerere, Tanu Warioba, amesema majeruhi huyo anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.