Dar es Salaam. Ziara ya saa nne ya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene jana iliibua suala la bajeti ya chakula ya Sh850,000 kwa kila mbwa anayefanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam, sawa na wastani wa Sh28,000 kwa siku.
Katika ziara hiyo, Simbachawene alibaini mbwa wawili kati ya saba wanaohudumiwa na Kituo cha Jeshi la Polisi Bandari ya Dar es Salaam, hawapati bajeti yao badala yake wanategemea mgao wa bajeti ya mbwa wengine watano hivyo ametoa muda wa siku saba kuhakikisha mbwa hao wanapata bajeti yao.
“Bandari hii(Dar es Salaam) ndio kitovu cha uchumi wetu, lakini isiposimamiwa vizuri inaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa hiyo askari muhimu hapa ni mbwa, nimewatembelea nimeona wapo wawili hawana bajeti ya chakula na wanagawana chakula na wengine,” alisema Simbachawene.
“Nimetoa siku saba wapate bajeti yao kwa sababu thamani yake ni sawa na askari,wanafanya kazi ambazo hata binadamu hawezi kuzifanya kwa hiyo kila mbwa apate chakula chake.”
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Polisi Bandari Tanzania, Benedict Mwapujila aliyepokea agizo hilo alisema mchanganuo wa bajeti hiyo kwa mbwa mmoja inahusisha vyakula maalumu ambavyo ni vidonge vya Pelles vyenye virutubisho vyote muhimu, vifaa vya usafi na dawa maalumu kwa ajili ya afya yake.
Pia, Mwapujila alisema majukumu ya mbwa hao kila siku bandarini ni kunusa kila mzigo unaoingia kutoka nje ya nchi na wana uwezo wa kutambua mzigo uliobeba nyara ikiwamo silaha, mabomu, pembe za ndovu, magamba ya kakakuona na dawa za kulevya kama heroin, bangi na cocaine.
Mwapujila alifafanua zaidi kuhusu maisha na utendaji kazi wa mbwa hao akikiri kuishi maisha ya kutegemea mgao wa chakula kutoka kwa wenzao.
“Ni mwaka mmoja tangu tulipowanunua nchini kwa wafugaji, hawajasajiliwa na hawana majina hadi wamalize mafunzo.
“Mbwa wengine wanne kati ya watano tuliwanunua muda mrefu kutoka Marekani lakini hao wawili tuliona tuwatafute hapa hapa na tuwafundishe. Kazi yao kubwa sana ukitaka kupima utendaji wao kwa sababu uwepo wao tu unachagiza watu kuogopa kupitisha vitu hivyo,” alisema Mwapujila.
Simbachawene aliyeanza ziara hiyo saa 3:00 asubuhi katika ofisi za Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, alitembelea ofisi za Polisi Wanamaji Kanda ya Dar es Salaam kabla ya saa 5:00 asubuhi na kufika ofisi za Kikosi cha Polisi Bandari Tanzania, kilichopo Mamlaka ya Usimamizi wa. Bandari Tanzania (TPA).
Malengo ya ziara hiyo itakayofikia ukomo wake kesho ni kukagua na kutathimini utendaji kazi wa vikosi vyote vya Jeshi la Polisi katika kanda ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Awali, baada ya kikao cha ndani na maofisa wa jeshi hilo, Simbachawene alieleza kufurahishwa na kazi kabla ya kukabidhi zawadi ya gari jipya Land Cruiser aina ya GX-V8 kwa Kamanda Lazaro Mambosasa wa kanda hiyo ili kuongeza kasi ya utendaji.
“Kama nilivyosema hali ya uhalifu imepungua hata makosa ya trafiki yamepungua kwa hiyo imesaidia na umeonekana (Lazaro Mambosasa) nikupongeze kwa zawadi ya Krismasi tena kutoka kwa Rais mwenyewe(Rais John Magufuli) ,” alisema Simbacheweme.