Baraza la Seneti lapokea mashtaka dhidi ya Trump


Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani limewasilisha hati ya mashtaka mbele ya Baraza la Seneti dhidi ya rais wa zamani Donald Trump na kufungua njia ya kuanza kwa shauri la pili la kihistoria.

Wawakilishi tisa walioteuliwa kuongoza mchakato huo wamewasilisha shtaka moja pekee linalomtuhumu Trump "kuchochea uasi" baada ya wafuasi wake kuvamia majengo ya Bunge mjini Washington mapema mwezi huu.


Wakitembea kwa mwendo wa polepole wawakilishi hao waliwasilisha hati ya mashtaka mbele ya Baraza la Seneti na kufungua njia ya kuanza kwa shauri la kihistoria kwa kiongozi wa taifa hilo kushtakiwa mara mbili na Bunge.


Mwakilishi wa jimbo la Maryland Jamie Raskin  ndiye alisoma shakta dhidi ya Trump ndani ya ukumbi wa Baraza la Seneti, ambako rais huyo mstaafu bado uungwaji mkono kutoka maseneta wa chama chake cha Republican.


Kuwasilishwa kwa hati hiyo ya mashtaka iliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi linaloongozwa na chama cha Democrat mnamo Januari 13 kunafungua njia ya kuanza kwa shauri dhidi ya Trump katika wiki ya pili ya mwezi Februari.


Kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer amesema wajumbe 100 wa baraza hilo ambalo watafanya kazi kama mahakimu wataapishwa leo Jumanne na tayari wito wa kufika mbele ya baraza umetumwa kwa Bw. Trump.


Wanasiasa wa Democratic na Republican walikubaliana kuchelewesha kwa muda wa wiki mbili kuanza kwa shauri hilo ili kumruhusu Trump kuandaa utetezi wake dhidi ya shtaka linalomkabili la "kuchochea uasi" na kuruhusu Baraza la Seneti kuidhinisha wateule wa nafasi mbalimbali za utawala rais Joe Biden.


Mara hii kesi hiyo itaongozwa na makamu mwenyekiti wa Baraza la Seneti Patrick Leahy kutoka chama cha Democratic ambaye ni seneta mkongwe zaidi badala ya jaji mkuu wa Marekani John Roberts aliyeongoza shauri la kwanza dhidi ya Trump wakati alipokuwa rais.


Makamu mwenyekiti wa Baraza la Seneti kwa kawaida ndiye huongoza mashtaka dhidi ya kiongozi yeyote asiye rais wa Marekani ambaye shauri lake limewasilishwa mbele ya chombo hicho.


Wakati hayo yakijiri, rais Joe Biden ameonesha kutojishughulisha kabisa na kile kinachoendelea Bungeni dhidi ya mtangulizi wake na shauri linalomkabili.


Wanasiasa wa chama cha Biden wameendelea kutoa wito wa Trump kuwajibishwa kwa kile wanasema alichochea uasi dhidi ya utawala wa Marekani.


Mwakilishi wa chama cha Democratic Jerry Nadler ambaye pia ni mwenyeketi wa kamati ya mahakama yaBaraza la Wawakilishi amesema sasa ni wajibu kwa Baraza la Seneti kufanya kazi yake kwa kumtia hatiani Trump na kumzuia kutowania tena wadhifa utakaomwezesha kusababisha madhara kwa taifa hilo.


Wawakilishi 10  kutoka chama cha Republican walijiunga na wenzao wa Democratic kupiga kura za ndiyo za kumfungulia mashtaka Trump kwa kuchochea wafuasi wake kuvamia majengo ya bunge mnamo Januari 6 ili kuzuia kuidhinishwa kwa Biden kufuatia ushindi aloupata kwenye uchaguzi wa Novembva 3 mwaka uliopita.


Watu watano walikufa katika vurumai hiyo ikiwemo afisa mmoja wa polisi na mwandamanaji aliyepigwa risasi na mlinzi wa majengo ya Bunge.


Hii ni mara ya pili kwa Trump kufunguliwa mashtaka. Mwaka mmoja uliopita Bunge lilimshtaki Trump ili kumuondoa madarakani kwa kuishinikiza Ukraine kufanya uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa wakati huo Joe Biden.


Hata hivyo Baraza la Seneti lililokuwa chini ya udhibiti wa Republican lilimuondolea hatia kiongozi huyo.


Katika shauri la sasa maseneta wa  Republican karibu 17 wanatarajiwa kupiga kura kuunga mkono mashtaka dhidi ya Trump.


Iwapo atapatikana na hatia, Baraza la Seneti linaweza kumpiga marufuku ya kushika tena madaraka, hatua itakayomzuia kuwania tena urais mwaka 2024.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad