Kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Amon Kakwale amekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba limesitisha tamasha la “Tumewasha na Tigo” linaloandaliwa na Wasafi Media kwa sababu za kiusalama.
Taarifa hizo ambazo Kakwale ameziita za uzushi zimesambaa mitandaoni leo Januari 30 zikionyesha barua yenye taarifa zote muhimu za jeshi la polisi kama vile nembo, muhuri, jina na sahihi. Kamanda Kakwale amesema tamasha hilo lipo, litaendelea kuwepo na Jeshi la Polisi litatoa ulinzi kama kawaida.
“Hiyo barua si ya kweli, tamasha lipo na litapewa ulinzi na Jeshi la Polisi kama ilivyo kwa matamasha mengine,” amesema kamanda.
Aidha, kamanda huyo amewakemea watu wenye tabia ya kugushi barua kama ilivyofanyika kwa hiyo na kuwataka waache mara moja. “Si jambo zuri kugushi barua namna hii. Hiki kilochofanyika ni matumizi mabaya ya ofisi,” amesema.