MFANYABIASHARA na mmliki wa Kampuni ya Alibaba, Jack Ma, nchini China, kwa mara ya kwanza leo amejitokeza hadharani kuzungumza na walimu kwa njia ya video, ikiwa ni miezi miwili tangu alipodhaniwa kupotea baada ya kukosoa mfumo wa kisheria wa China unaokwamisha biashara.
Taarifa iliyochapishwa kupitia mtandao wa takwimu wa ‘Forbes’, imeeleza kuwa Ma amelazimika kujitokeza hadharani kutokana na ulazima wa kuzungumza na walimu wa vijijini ambapo imekuwa ni kawaida yake kila mwisho wa mwaka kufanya hivyo ili kutambua idadi na mchango wa walimu hao.
Ma hajatokea hadharani au kutuma chochote katika mitandao ya kijamii tangu Oktoba mwaka jana, ikiwa ni wiki moja kabla ya kampuni tanzu la kifedha la Alibaba, liitwalo Ant Group, likiwa limepangwa kujiorodhesha katika soko la fedha la Hong Kong.
Ma, ambaye aliwahi kuwa mwalimu wa Kiingereza, alifanya elimu msingi wa taasisi yake, jambo ambalo amekuwa akilishughulikia zaidi tangu kustaafu kwake kutoka Alibaba mwaka 2019. Kupotea kwake kulizua mtafaruku mkubwa mnamo wiki kadhaa zilizopita.
Alibaba ni moja ya makampuni maarufu ya teknolojia nchini China lakini likiwa linakabiliwa na changamoto nyingi kutoka serikali ya China.