Mtendaji Mkuu wa Simba (C.E.O), Barbara Gonzalez.
MTENDAJI Mkuu wa Simba (C.E.O), Barbara Gonzalez, amemtaja kocha atakayekuja kumrithi Sven Vandenbrock ni yule atakayekidhi vigezo ambavyo wameviweka.
Barbara alisema kocha atakayepewa nafasi ya kuliongoza benchi la ufundi la timu hiyo ni yule mwenye leseni ya daraja la juu, uzoefu kwenye masuala mbalimbali ya ukocha ikiwemo kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwemo uzoefu wa kufundisha timu za taifa.
Barbara amesema mpaka sasa wamepokea maombi ya makocha 55 kutoka mataifa mbambali, ikiwemo Serbia, Ufaransa, Ureno pamoja na nchi nyingine nyingi zilizoendelea kisoka na kuweka wazi kuwa wakimpata mtu sahihi huenda akamtangaza hata ndani ya siku tano zijazo lakini kinyume na hapo wataendelea kusubiri.
“Kwa sasa kuna walimu 55 ambao wameomba kazi na bado tunachambua CV zao hadi tupate kocha sahihi kwa ajili ya timu yetu. Unajua kwenye kuchagua kocha lazima uchukue muda ili upate mtu sahihi.“
Rene Wailer
Ukianza kuharakisha jambo unaweza ukaharibu msimu mzima pamoja na mipango ya ‘Champions League’, kuna makocha kutoka Serbia, Ufaransa yupo pia kutoka Portugal na wengine wengi,” alisema Barbara.
Mpaka sasa makocha wawili wanatajwa kutakiwa zaidi na Simba, makocha wote hao wanakidhi vigezo ambavyo Barbara amevitaja.
Makocha hao ni Florent Ibenge anayeinoa AS Vita ya DR Congo na Rene Wailer aliyewahi kukinoa kikosi cha Al Ahly.
Stori: ISSA LIPONDA,Dar es Salaam