PERFECT Chikwende, nyota mpya wa Simba amesema alitumia muda wa mwezi mmoja kuwasoma wapinzani wakubwa wa Simba ambao ni Yanga na Azam FC.
Chikwende amejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na tayari ameanza mazoezi na kikosi hicho kinachojiandaa na mechi za Simba Super Cup, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Nyota huyo ambaye amekabidhiwa jezi namba 23 iliyokuwa ikivaliwa na Charles Ilanfya aliyepelekwa KMC kwa mkopo, amesema akiwa Zimbabwe, alikuwa akiifuatilia Ligi ya Bongo zikiwemo mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga jambo ambalo linamfanya asiwe na hofu na wapinzani wake hao.
“Ninawajua vema wapinzani wangu ambao ni washindani wakubwa wa Simba, niliwafuatilia kwenye mechi zao za nyuma ambapo Yanga niliwatazama walipocheza na Azam, pia niliifuatilia mechi ile ya Azam na Simba.
“Kwa takribani mwezi mmoja, nilikuwa nafanya kazi ya kuwaangalia namna wanavyocheza na nimeona uwezo wao, hivyo nipo tayari kukabiliana nao.“Tangu nianze mazoezi na wenzangu, naona timu ipo vizuri, nina imani nitazoea mazingira na kufanya vizuri katika maisha yangu mapya,” alisema Chikwende na kuongeza.
“Maleno yangu ni kuisaidia Simba kwenye kila michuano ambayo inashiriki iwe ya ndani au ya kimataifa, kikubwa mashabiki watuunge mkono na nina imani tutafanya vizuri.”