ABIRIA kutoka Marekani kwenda Uingereza wamekataliwa kupanda ndege leo (Jumatatu) baada ya matokeo ya vipimo vyao kuhusu ugonjwa wa Covid-19 kutiliwa shaka licha ya serikali kusema kwamba vikubaliwe.
Wakati huohuo, kulikuwa na vurugu kubwa kwa abiria wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Hearthrow jijini London, kwani walilazimika kusubiri kwa saa tatu katika misururu baada ya ofisi zinazoshughulikia usafiri kufungwa kwa muda wa wiki nne zijazo.
Matokeo yake wasafiri wanabidi kuwa chini ya karantini katika mahoteli kutokana na kufungwa kwa ofisi hizo.
Hannah Holland ( 23) mkazi wa Sheffield, Uingereza, aliangua kilio alipokataliwa kupanda ndege ya shirika la American Airlines (AA) kutoka Philadelphia kupitia uwanja wa ndege wa O’Hare, Chicago, nchini Marekani, ambayo ilikuwa itue London alfajiri hii.
Mwanamke huyo alikuwa na hati iliyomwonyesha kwamba hakuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Covid, hati ambayo ilionyesha vipimo vilichukuliwa saa 72 kabla ya saa za kuondoka, lakini wafanyakazi wa AA walisema hati hiyo haitoi ruhusu kusafiri kwenda Uingereza licha ya kwamba vipimo vilivyofanywa vinakubalika na serikali ya Uingereza.
Gazeti la MailOnline pia limegundua kwamba wafanyakazi wa shirika la ndege la Uingereza, British Airways na AA katika uwanja wa ndege wa Heathrow wamekuwa wakiwarudisha abiria wanaotaka kusafiri kwenda Marekani kwa kutokamilika kwa vipimo vinavyoonyeshwa kwenye hati zao.
Utaratibu huo umeanza leo saa 10 za alfajiri kwa kufunga ofisi zote za safari na watu wanaowasili uwanjani kuwekwa katika karantini ya siku 10 au siku tano iwapo watafanyiwa kipimo kipya na kuonekana hawana maambukizi.
Pia umeanza wakati wasafiri wote wanaoingia Uingereza kulazimika kukaa katika mahoteli chini ya mipango ya kuifunga mipaka ya Uingereza kutoka leo hadi Februari 15 ili kuweka karantini ya lazima nchini kuhakikisha hakuna mfumko mpya wa Covid-19 nchini humo.
Katika kuupiga vita ugonjwa huo, raia zaidi ya milioni tano watapatiwa chanjo ya ugonjwa huo tangu leo, wengi wao wakiwa ni watu wenye umri zaidi ya miaka 70.
Takwimu za tiba nchini Uingereza zinaonyesha kwamba mtu mmoja kati ya sita waliowasili nchini humo hawakuwa na maambukizi lakini waliyapata tangu Septemba mwaka jana.
Aidha, vifo 671 vimerekodiwa nchini humo juzi (Jumapili), ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kutajwa katika siku za Jumapili, ambapo matukio mapya ya maambukizi yamefikia watu 38,598.