Cristiano Ronaldo ameweka rekodi ya kuwa kinara wa ufungaji mabao kwenye historia ya mpira wa miguu duniani, amefikisha magoli 760, baada ya kufunga kwenye mchezo wa fainali ya Italia Super Cup dhidi ya Napoli, mchezo ambao Juventus wameshinda kwa mabao 2-1.
Ronaldo alifunga bao lake la 760 dakika ya 64 kwenye mchezo huo wa fainali dhidi ya Napoli, mchezo ambao Juventus walishinda kwa mabao 2-0 ambapo bao jingine la Juventus lilifungwa na Alvaro Morata dakika ya 90. Goli hilo limemfanya Ronaldo kuwa mfungaji bora wa muda wote katika michezo rasmi kwenye historia ya mpira wa miguu.
Awali Nohodha huyo wa Ureno alikuwa na idadi sawa ya mabao (759) na mshambuliaji Josep Bican, ambaye aliwahi kuvichezea vilabu vya Rapid Vienna, Slavian Prague na timu ya taifa ya Czechoslovakia.
Katika idadi hiyo ya mabao Ronaldo amefunga mabao mengi zaidi 450 akiwa na klabu ya Real Madrid ya Hispania lakini pia aliifungia Manchester United ya England mabao 118, na bao alilofunga jana lilikuwa la 85 akiwa na kikosi cha Juventus na mabao 102 amefunga akiwa na kikosi cha timu yake ya taifa ya Ureno.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35 amefunga mabao mengi zaidi kwa mguu wake wa kulia mabao 488, mguu wa kushoto mabao 139, mabao 131 amefunga kwa kichwa, huku mabao aliyofunga kwa penati ni mabao 133.
Na mchezaji pekee anayetizamiwa huenda akafikia rekodi hii ni mshambuliaji wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi ambaye kwa sasa ana mabao 715 na amezidiwa miaka 2 na Ronaldo.