Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Festo Kiswaga, amemkamata na kumuweka ndani Meneja wa Kampuni ya Madini ya EMJ, inayomilikiwa na kiongozi wa CCM, kwa madai ya kukwepa kulipa kodi za Serikali, katika Mgodi wa Dutwa wilayani humo.
Kiswaga, ameamuru kuwekwa ndani Meneja wa Kampuni ya EMJ, Juvenari Mrashan, baada ya kufanya ziara mgodini hapo ambapo inadaiwa kampuni hiyo inayomilikiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM-NEC) Taifa, na kukwepa kulipa kodi ya mrabaha kwa siku tatu, pamoja na ushuru wa halmashauri unaodaiwa kufikia Sh. Milioni Nane.
“Na taarifa kwamba usiku siku za wikiendi haturuhusu kutoa mawe lakini kampini hii mnatoa mawe, na mmoja yam awe mliyotoa yalikuwa ya wizi mliibiana wenyewe kwa wenyewe kesi ishafika kwa mkuu wa mkoa, lakini tulikubaliana kuhusu kulipa ushuru wa halamashauri matokeo yake mpaka sasa hivi mnatoa mifuko bila kulipia ushuru”, amesema.
Kwa upande wake meneja wa kampuni hiyo alisema hawezi kulitolea maelezo suala hilo mpaka atakapo pitia taarifa za muhasibu kwani ndiye anayehusika na malipo hivyo kuomba apewe muda kwa ajili yakufuatilia taarifa hizo ndio atoe majibu juu ya malipo hayo.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya alishangazwa na kitendo cha meneja huyo kutokujua taarifa za malipo katika mgodi huo hivyo kuamuru meneja huyo kuwekwa ndani mpaka fedha za mifuko 6,442 zitakapolipwa.
Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Simiyu, Oscar Kaloa, amewataka wanunuzi wa madini kufanyakazi hiyo kwa kufuata sheria huku akisisitizia suala lakupata kibali kwa ajili yakusafirisha madini kiuhalali.