Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Sousa ameshinda muhula wa pili wa miaka 5 katika uchaguzi uliofanyika jana Jumapili chini ya kiwingu cha janga la virusi vya corona.
Wakati asilimia 99 ya kura ikiwa imekwishahesabiwa, de Sousa amepata asilimia 61 dhidi ya wapinzani wake wawili wa karibu waliovuna chini ya asilimia 15 ya kura.
Hata kabla ya uchaguzi wa jana, mwanasiasa huyo anayegemea sera za mrengo wa kulia alikuwa anaongoza kwa wingi mkubwa katika kura za maoni ya umma licha ya wasiwasi kwamba janga la COVID-19 lingeuteteresha ushindi wake.
De Sousa amewavutia sehemu kubwa ya wapiga kura wa Ureno kwa jinsi anavyoshirikiana na serikali ya waziri mkuu Antonio Costa kushughulikia kadhia ya Corona na kutoa umuhimu kwa utulivu wa kisiasa nchini humo.