Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic, amesema kuwa ameyapokea maagizo ya Rais Magufuli, na kwamba walikwishaanza kuchukua hatua za ujenzi wa shule ya msingi King’ongo ikiwemo kutenga milioni 80, baada ya wao kuona video ikionesha changamoto ya shule hiyo.
Kauli hiyo ameitoa jana Januari 18, 2021, zikiwa zimepita saa kadhaa tu tangu Rais Dkt. Magufuli, alipotoa maagizo ya kwamba akija Dar es Salaam, akute ujenzi wa shule hiyo umekamilika na wanafunzi hawakai chini, huku akishangazwa na viongozi wa mkoa huo wapo lakini hawashughulikii kero hiyo.
“Awali ya yote nimeyapokea maelekezo ya Mhe. Rais, sisi tangu tulipoona hiyo clip hatukukaa kimya kila mtu alishangaa kwa sababu ni taarifa ambazo hazikuwahi kufika ofisini kwangu.
“Tayari kazi ya kuchimba misingi imeanza, kikubwa tunachofanya ni kupata fundi ambaye atakamilisha hii kazi kwa muda mfupi unaowezekana na ubora unaotakiwa, lakini tumeshaweka oda kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
“Tangu jana (juzi) mimi na timu tupo ‘site’ na leo (jana) asubuhi mkuu wa wilaya amefika lakini kama manispaa tunahamisha haraka sana milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 4 na madawati hapa ninavyoongea na wewe nipo site,” amesema Beatrice Dominic, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo.
Aidha, uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge umeanza kutekeleza agizo hilo.
Tayari vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo vimekwishafikishwa katika eneo husika, na Mkuu huyo wa mkoa ameagiza kazi ya ujenzi kufanyika usiku na mchana chini ya usimamizi wake. Ameagiza kujengwa kwa vyumba vinane vya madarasa na kubomolewa kwa vyumba vya madarasa ambavyo ni chakavu na kujengwa upya.
Mapema jana akizindua shule ya sekondari ya Wavulana ya Ihungo iliyopo mjini Bukoba, Rais Dkt Magufuli aliwaagiza Viongozi wa wilaya ya Ubungo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha atakaporejea jijini Dar es salaam, madarasa katika shule hiyo ya msingi ya King’ongo yawe yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini.
Wanalala maofisini tu hawatembei kupata changamoto za wananchi wanasubli hadi vyombo vya habar
ReplyDelete