MTAYARISHAJI wa muziki wa Marekani na rapa wa miondoko ya Hip Hop, Andre Romelle Young, maarufu kama ‘Dr. Dre’, ameruhusiwa kutoka kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kuzidiwa na kulazwa kwa siku kadhaa katika hospitali ya Cedars-Sinai Medical Center, Los Angeles, Marekani, baada ya mshipa kwenye ubongo kutanuka.
Mtandao wa Tmz umeripoti kuwa huenda chanzo cha ugonjwa huo ni msongo wa mawazo kutoka kwa aliyekuwa mke wa rapa huyo, Nikole Young, ambaye alidai talaka mwezi Juni 2020 sambamba na kiasi cha Dola za Marekani mil. 2 sawa na zaidi ya sh. bilioni 4 za Tanzania kama fidia, na mpaka mchakato wa talaka utakapomalizika Dre atakuwa anamlipa dola laki 300 sawa na zaidi ya sh. mil 600 kila mwezi.
Kwenye ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa Instagram, Dre amewashukuru wafanyakazi wote wa kituo cha Cedars Sinai Medical Center kwa matibabu waliyompa, mashabiki na familia ambao walikuwa wanamwombea, na kuongeza kuwa anaendelea vizuri na anaamini siku chache zijazo atatoka hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa gazeti la Forbes, Dr. Dre ana utajiri wa zaidi ya trilioni 1, na nje ya muziki rapa huyo anafanya biashara ambazo zimemwingizia mkwanja mrefu, kama ile ya headphones za Beat by Dre ambayo baadaye aliiuza kwa kampuni ya Apple mwaka 2014.
Dre anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa muziki wa Hip Hop akifanikisha kutengeneza ‘beat’ za nyimbo za wasanii wa Hip Hop kama Eminem, 50 Cent, The Game Snoop Dogg.