Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe, amesema kuwa zoezi la ukaguzi wa magari yanayotoka nje ya nchi litaanza kutekelezwa mara moja ifikapo Machi 1, 2021, huku lengo likiwa ni kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa nchini zina ubora unaohitajika.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 26, 2021, wakati akitoa onyo kwa mawakala wakubwa wa mafuta ya kula nchini, kuacha kupandisha bei ya bidhaa hiyo kinyume na bei ambayo ni ya kawaida walioagizia kutoka nje ya nchi na ile ya viwandani.
Na kuongeza kuwa hivi karibuni Shirika la Viwango nchini (TBS), lilitangaza kuwa litaanza ukaguzi wa magari yote yanayoingizwa nchini kutoka nje ya nchi na yale yatakayobainika kutokuwa na ubora hayatoruhusiwa kuingia.
Aidha mbali na hayo Waziri Mwambe, ameongeza kuwa kwa sasa changamoto ya mafuta nchini imepungua kwani mafuta yapo yakutosha baada ya kuwasili kwa Meli mbili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ambazo zimeshusha mafuta takribani Tani 48,000 na uhitaji ukiwa ni mafuta Tani 30,000 kwa mwezi, huku akisema changamoto itakayoendelea kwa muda mfupi ni ongezeko la bei kwani mafuta yanayowasili tayari waagizaji walishaagiza kwa bei hii ambayo imepanda Duniani kote.