Wakazi wawili wa Kijiji cha kilimawe kata ya Mwantini mkoani Shinyanga, Mabuga Ndakuna (70) na Timotheo Mabuga ( 17) wamejeruhiwa na mnyama aina ya fisi wakati wakijaribu kuokoa mifugo yao iliyokuwa kwenye banda la nyumba yao isishambuliwe na mnyama huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana na kusema kuwa tukio hilo limetokea Januari 11 mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri ambapo fisi huyo alivamia banda la kuku katika familia ya Mzee Mabuga na kushambulia kuku ndipo katika harakati za kumfukuza alianza kuwashambulia.
“Mzee Mabuga Ndakuna aling'atwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani,miguuni na kuvunjwa mkono wa kushoto huku mwanae Timotheo aking'atwa sehemu mbalimbali za mwili wake kama vile mikono,miguuni na mabegani,”alisema Magiligimba.
Kamanda Magiligimba alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni mnyama huyo aina ya fisi kuvamia banda la kuku na wanafamilia hao kutoka nje kwenda kuokoa mifugo yao isiendelee kushambuliwa ambapo baada ya kutekeleza tukio hilo alikimbilia vichakani.
“Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, hali zao zinaendelea vizuri na jitihada za kumtafuta mnyama huyo zinaendelea ili kuwaondoa wanyama wakali katika kijiji hicho kwa kushirikiana na maafisa wanyama pori,”alisema Magiligimba.
Mwisho.