KAMA ilivyo kawaida yake kuibua mambo mazito ya kumfanya azungumziwe au ‘kutrendi’, staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ ameliibua tena.
Harmonize au Harmo amejikuta akichezea za uso baada ya kutamba na kuwatakia Heri ya Krismasi na kutambua nguvu ya waliowahi kuwa wapenzi wa aliyekuwa bosi wake kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdu ‘Diamond Platnumz’.
Baadhi ya wanawake hao ambao ni ‘maeksi’ wa Diamond au Mondi au wengine ambao waliwahi kuwa na ukaribu na jamaa huyo ni pamoja na mastaa wa Bongo Movies, Jacqueline Wolper Massawe, Wema Isaac Sepetu, Kajala Masanja, Aunt Ezekiel na Irene Uwoya.
Wengine ni baby mama wa Mondi, mwanamitindo Hamisa Mobeto, Gift Stanford ‘Gigy Money’, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, Mariane Mdee ‘Mimi Mars’ na wengine.
AANZA NA WEMA
Harmo alianza kumposti Wema kwenye Insta Story ya ukurasa wake wa Instagram na kumtakia Heri ya Krismasi na kumweka kwenye listi ya Nguvu ya Mwanamke ambapo mwanadada huyo naye aliipokea kwa ‘ku-riposti’ kwenye ukurasa wake wa Instagram kuonesha kwamba ameikubali.
Ikumbukwe kwamba, Wema ni zilipendwa wa Mondi hivyo kitendo hicho kimeibua hisia tofauti kwa mashabiki wao.
KAJALA
Mbali na Wema, pia Harmo alimposti Kajala kwenye listi yake hiyo na kuamsha tena ile skendo inayosambaa kama moto wa kifuu kwamba wanatoka kimapenzi.
Hivi karibuni kumekuwa na stori nyingi zikiwahusisha Harmo na Kajala kuwa ni wapenzi, lakini kila mmoja amekuwa akikanusha kwa wakati wake.
Inafahamika kwamba, Kajala aliwahi pia kuwa na ukaribu na Mondi japokuwa hakuna uthibitisho kama walikuwa wapenzi, lakini kitendo cha Harmo kuwa na ukaribu na mwanamama huyo inasemekana ni sehemu ya kumtafuta uchokozi bosi wake huyo wa zamani.
UWOYA
Kwenye listi hiyo ya Harmo aliyoipa jina la Nguvu ya Mwanamke, yupo pia mwanamama Uwoya ambaye amekuwa na ukaribu na mastaa wengi Bongo.
Hata hivyo, baadhi ya watu wameendelea kumsema vibaya Harmo wakimwambia kwa kufanya hivyo ni kumchokoza Mondi ambaye Uwoya ni mtu wake wa karibu na waliwahi kutajwa kuwa wanatoka kimapenzi.
AUNT
Kutoka kwa Uwoya aliyefuata kwenye listi hiyo ya Harmo ni mwanamama Aunt Ezekiel ambaye inafahamika kwamba ni mtu wa karibu wa Mondi na Wasafi kwa jumla.
Kitendo cha Harmo kumposti Aunt kinatajwa kutaka kumvuta upande wake ilihali ikifahamika ana ukaribu na Mondi.
MOBETO
Harmo pia amemposti Mobeto katika kuonesha Nguvu ya Mwanamke ilihali ikifahamika kwamba, mwanamama huyo ni mzazi mwenza wa Mondi ambaye amezaa naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Dyllan.
Hata hivyo, miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na skendo mtaani kwamba, Harmo ana ukaribu wenye viulizo na Mobeto ilihali akijua kuwa, mwanamama huyo alikuwa ni ‘chombo’ cha bosi wake huyo.
SHILOLE
Pia kwenye listi hiyo, Harmo alimuweka mwanamama Shilole ambaye ni miongoni mwa watu wa karibu wa Mondi.
Mara kadhaa, Shilole au Shishi Baby amekuwa akishirikiana kwa karibu na Mondi na mfano mzuri ni hivi karibuni tu ambapo jamaa huyo alimpeleka Le Grand Mopao Koffi Olomide kwenye mgahawa wa mwanadada huyo uliopo pale Ada Estate, Kinondoni jijini Dar.
Kitendo cha Harmo kutengeneza ukaribu na Shilole kinatajwa kutaka kuvuruga ukaribu wa mwanamama huyo na Mondi.
WOLPER
Kwenye listi hiyo pia yumo Wolper ambaye inafahamika kwamba ni ‘eksi’ wake na hivi karibuni kumekuwa na maneno mengi huku kila mmoja akijipanga kujibu mapigo kwa mwenza.
Miezi kadhaa iliyopita akiwa stejini jijini Dodoma, Harmo alikiri kwamba aliachana na Wolper kwa sababu alikuwa ni mpenzi wa Mondi.
Kitendo cha kumposti Wolper kwenye listi hiyo kinatajwa kuwa ni mwendelezo uleule wa kumchokonoa Mondi.
MIMI MARS
Inafahamika kwamba, miezi kadhaa iliyopita, Mimi Mars alihusishwa kuwa na ukaribu na Mondi. Ukaribu wao ulikwenda mbali zaidi na kudaiwa kuwa huwenda kuna uhusiano wa kimapenzi baada ya Mimi Mars kuonekana akiogelea kwenye bwawa nyumbani kwa Mondi.
Huku akijua ukaribu huo, Harmo pia amemtaja Mimi Mars kwenye listi yake hiyo na kuonesha kwamba ni mwendelezo uleule wa kumchokonoa Mondi.
UTETEZI WA HARMO
Katika utetezi wake, Harmo anasema yeye alichoangalia kwenye listi hiyo ni kumshukuru kila mwanamke aliyemuunga mkono kwa mwaka 2020 kwa kuwa anajua jinsi ambavyo wana nguvu kwenye jamii.