Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete amefunguka kuhusu upande wa pili wa maisha yake nje ya siasa huku akiahidi kuwa kitabu chake kitakachotoka kabla ya Juni kitazungumza kwa kina zaidi.
Kikwete ambaye alisema haoni aibu anapofika sehemu ya watu wengi, alieleza hayo katika mahojiano maalumu yake na Salama Jabir katika kipindi chake cha Salama kinachorushwa na mtandao wa Youtube.
Alisema kazi ya kuandika kitabu hicho inaendelea na iko katika hatua za mwisho “sijui ni lini lakini sidhani kama itavuka nusu ya mwaka 2021, kitakuwa kimekamilika na kitakuwa katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili.
“Kuna mengine wakati mwingine hayasemekani au huwezi kuyasema lakini kuna mengi ambayo nadhani hayana usiri huo, nayo nimejaribu kuchangia katika kitabu changu kile ninachokiandika na itasaidia watu wengi kujua ilikuwaje hadi uamuzi huu ukafikiwa, chanzo chake ni nini, kuna baadhi ya mambo ambayo yatasaidia jamii,” alisema.
Hakuna kama Msoga
Katika mahojiano hayo, Kikwete aligusia nyumbani kwake Msoga, akisema anapapenda sana kuliko sehemu nyingine yoyote na akiwa huko anaishi maisha ya kawaida akifanya kile anachostahili kufanya kwa jitihada zake.
Kuhusu iwapo anajua kuwa watu wanampenda, Kikwete ambaye hakuulizwa wala kuzungumzia masuala ya kisiasa, anasema “Sijui kama napendwa ila najua kuwa sichukiwi, sina ushahidi wa kuchukiwa.”
Shuleni na msuli
Rais huyo kwa miaka 10 kuanzia 2005 hadi 2015, alisema baba yake mzazi aliyekuwa mfanyakazi wa Serikali, alimpeleka shule mara ya kwanza Lushoto 1956.
“Lakini kwa kuwa nilikuwa mdogo, siku moja mwalimu aliniambia wewe kesho usije shule, nikafurahi maana nilikwenda shule kwa sababu dada zangu wawili ninaowafuata walikuwa shule, kwa hiyo sikuwa na mtu wa kucheza naye.
“Kubanwa darasani kwa muda mrefu nako kulikuwa hakunifurahishi kwa hiyo niliona sawa tu.
Alisema baadaye baba yake alihamishiwa Same naye akaanza kusoma huko lakini baada ya utundu kuzidi alizungumza na babu yake wakaafikiana arudi kijijini akae na babu yake hadi alipoanza tena darasa la kwanza mwaka 1958.
Anasema hapo napo alisoma kwa muda lakini kulikuwa na kijana mmoja anaitwa Kivuli ambaye alikuwa anacheza naye, alikuwa hajapelekwa shule alienda shule baadaye akachoka akaamua kutokwenda shule.
“Asubuhi navaa uniform (sare) lakini naenda kwa rafiki yangu (Kivulini) pale jirani tunacheza, wakikaribia kutoka na mimi natoka tunarudi nyumbani, kama vile na mimi nimetoka shule baadaye babu kaambiwa, akanivizia asubuhi akanikamata nimevaa msuli wangu nimeamka.
“Kama nilivyokuwa, akaniambia twende shule nikamwambia nivae shati akasema hapana leo hata shati hauvai twende, basi tukaenda akanichapa fimbo mbili, toka siku ile sikukosa tena shule na uzuri nilikuwa nimefanya hivyo kwa muda mfupi na baada ya hapo niliendelea tu vizuri na nikapenda sana kusoma.” anasimulia.
Alisoma darasa la kwanza hadi la nne Msoga, shule ya kati Lugoba, kisha Sekondari Kibaha, Tanga School kidato cha tano na sita kisha mwaka 1972 akaingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi 1975.
Mlenda humwambii kitu
Kikwete alisema yeye anakula vyakula vya kawaida tu lakini akiwa kijijini kwao anapendelea zaidi kula ugali wa mtama na mlenda
“Kuna aina fulani ya mlenda mnangu, sisi tunaita hombo la mnangu, napenda kula kila siku, wengine watakula ubwabwa na nini lakini hicho ndicho chakula nimekuwa nakula na babu yangu na nimezoea kula,” anasema.
“Sisi katika mila zetu watoto wa kiume hawafundishwi kupika, wanafundishwa watoto wa kike, wa kiume wakikuona jioni wanakushangaa wewe unafanya nini, hizo ni mila zetu lakini mambo yamebadilika siku hizi.”
“Hayo mambo ya siku hizi ya mke na mme mnagawana siku za kupika wala sitaki kuingilia kwenye mambo hayo, ila mie siko huko, mie bado mtu yule wa zamani sana. Kwamba leo darling na wewe zamu yako ya kupika heheh wala sidhani kama Mama Salma atanipeleka huko maana kazi yake ya kwanza itakuwa kunifundisha kupika,” alisema Kikwete ambaye kushindwa kwake kupika kulimpa wazo la kuoa.
Wazo la kuoa
Anasema Tanu ilipounganishwa na ASP mwaka 1977, yeye alikuwa ofisa wa pili wa chama kwenda Zanzibar baada ya Kanali Ayubu Simba, kwa kuwa naye alikuwa katika mchakato wa kuunganisha vyama hivyo, yeye akishughulikia kuunganisha mifumo na kusimamia utawala katika ofisi ya Kisiwandui kuanzia mwaka 1977-1980 alipohamishiwa ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es salaam.
“Zanzibar pale lilianza tatizo la kwanza la kipindupindu, wakapiga karantini na mighahawa ikazuiwa, ikawa chakula kinapatikana katika hoteli za kitalii, Africa House, Bwawani na Zanzibar Hotel ambako alilazimika kula.
“Nikawa nakula kule lakini ikaanza kuwa ile hesabu ya fedha hailingani na maeneo yale ni ghali, kwa hiyo nikaona ngoja nijaribu kupika, kitu ambacho ni rahisi kwangu kupika ni chai, siwezi kupika ugali wala wali, nikaona pengine ni ndizi kwa hiyo nikaenda kununua ndizi nikawa nataka kuzikaanga.”
Aliongeza, “Nikawa najaribu kukumbuka wanavyofanya akina mama nikaweka mafuta na ndizi zangu nimeshazitengeneza kwa hiyo kabla ya kuweka ndizi mie nikaweka mafuta ulitokea mlipuko lakini niwahi kutoa uso wangu ,mengine yakarukia ukutani.
“Ile nyumba niliyokaa Kikwajuni mpaka leo bado ipo siku moja nikienda nitaingia nimuonyeshe anayekaa kuwa haya ni mafuta ya siku nilipojaribu kupika.”
Alisema baada ya pale aliamua kuajiri mpishi na kisha akapata wazo na kufanya uamuzi kuoa.
Alisema mke wake wa kwanza, Mamake Ridhiwani (marehemu) alikutanishwa na baba yake baada ya msichana wa kwanza, pia aliyekutanishwa na baba yake kugundulika na ujauzito.
“Siku nyingine tena kama mara ya kwanza, baba akaniambia twende, tukaenda nyumbani kwa bwana mmoja anaitwa Mwalimu Salumu, nikaonyeshwa mama yake Ridhiwan, unajua nimelelewa na wazazi wangu mimi, sikutaka kuingia kwenye zogo na mimi imani yangu ni kuwa mzazi hawezi kumuombea mwanawe jambo lisilokuwa na kheri, nikasema maadamu wazazi wamefikiria hivi ni sawasawa tu.”
Alisema baadaye mke wake huyo wa kwanza alifariki na alipohamishiwa Nachingwea ndipo akakutana na mke wake wa sasa, Mama Salma.
“Siku moja nimetoka nikawaona mabinti wawili wakiwa chuo cha ualimu pale, nikaona huyu Salma kama amekaa vizuri vizuri hivi, lakini nikawa sina namna ya kumfikia … siku moja natoka Nachingwea nadhani wao walikuwa wako likizo Lindi mjini nikamkuta wamesimama na rafiki yake nikasimama, nikamwambia karibu nimefikia mahali fulani akakataa kuja, akaniponda.”
“Lakini nikawa makini nafuatilia maendeleo yake akawa amemaliza chuo cha ualimu akaenda JKT Ruvu, hapo nikasema sasa hapahapa Ruvu kwa kuwa mie ni mwanajeshi na pale nina maafande wenzangu, nitakwenda. Nikaenda nikawaambia hapa nina mchumba wangu wakamwita akaja nikazungumza naye.”
Alisema Salma alipomaliza JKT aliajiliwa kule kwao Lindi naye akawa amehamishwa kutoka Nachingwea kwenda Masasi akawa anapita pale anamsalimia na baadaye akateuliwa kuwa naibu waziri na watu walikuwa hawajui kuwa hana mke kwani wakati huo alikuwa anawalea watoto, Salama na Ridhiwani.
“Baada ya kuwa naibu waziri nikahamia Dar es Salaa. Nikamwambia Salma sasa nataka kupeleka barua kwenu akasema peleka tu, nikapeleka barua ikajibiwa na baadaye tukafunga ndoa na sasa tuna miaka zaidi ya 30,” anasema.