Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amesema Vitambulisho kutolewa kwa uchache kulitokana na mchakato wa manunuzi ndani ya Serikali kwasababu mashine husika hainunuliwi ikiwa imefungwa pamoja, bali kila sehemu ya utendaji kazi ndani yake inakuwa na mkataba wake.
Ameongeza kuwa, Serikali inakusudia kufunga mashine mpya itakayozalisha vitambulisho 43,200 kwa siku badala ya ile ya awali inayozalisha vitambulisho 20,000.
Wananchi wengi waliojiandikisha wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa kupata vitambulisho kwa wakati badala yake wanapewa namba tu, huku baadhi ya maeneo wengine wakiwa hata namba hawana.
Idadi ya Watanzania waliotambuliwa hadi mwishoni mwa mwaka 2020 walikuwa milioni 18.5 lakini waliopewa vitambulisho Milioni 6.3 tu, ikimaanisha watu Milioni 12.2 milioni hawajapata Vitambulisho.