Dar es Salaam. Wakati mzee Seleman Hemed alipoamua kumkabidhi mwanae, Ally, gari aina ya Nissan Cetaro ili afanye biashara ya teksi na kumsadia kuendesha maisha yake hakuwaza hata kidogo kuwa zawadi hiyo ingegeuka chanzo cha kifo cha kikatili cha kijana huyo.
Kuuawa kwa Ally baada ya kupambana na waporaji wa gari hilo jijini Dar es Salaam usiku wa Novemba 9, 2013 na baadaye kukamatwa kwa wauaji hao wakiwa na gari hilo eneo la Chalinze, mkoani Pwani, ni ushahidi mwingine wa jinsi isivyo rahisi kwa damu ya mtu asiye na hatia kupotea bure.
Wiki iliyopita Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa ya mmoja wa wauaji hao, Msafiri Emmanuel Daniel, aliyekamatwa ndani ya gari aliloporwa Ally katika mji wa Chalinze mkoani Pwani siku tatu baada ya mauaji. Alikuwa akipinga kutiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa.
Mshtakiwa mwenzake, Jailos Aidan, ambaye pia alihukumiwa kunyongwa, alifariki siku chache kabla ya rufaa yao kusikilizwa mwishoni mwa mwaka jana.
Mke aingiwa mashaka
ADVERTISEMENT
Novemba 8, 2013, Ally aliondoka nyumbani kwake na kuendelea na kazi yake ya udereva teksi kama kawaida. Usiku ulipoingia, Ally hakurudi nyumbani, na hata siku iliyofuata hakurejea nyumbani wala kupatikana kwenye simu yake ya mkononi.
Hali hiyo ilimweka mke wake katika wasiwasi mkubwa kabla ya kuamua Novemba 9 kumfahamisha baba mkwe wake (baba yake Ally) kuhusu kutoonekana mumewe.
Baba yake Ally aliamua kuripoti wasiwasi huo katika Kituo cha Polisi Buguruni baada ya juhudi zote za kumtafuta kutozaa matunda.
Kama msemo wa Kiswahili “damu ya mtu haipotei bure” ndivyo unavyoweza kuelezea jinsi mfululizo wa matukio ulivyosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa.
Siku hiyo (Novemba 9, 2013) askari polisi mpelelezi aliyejulikana kwa jina la Doto aliripoti katika kituo chake cha kazi cha Buguruni kama kawaida na kukutana na taarifa za gari lililoonekana usiku uliotangulia ambalo mtu mwanaume alirushwa nje eneo la Kiwalani, huku gari hilo likiwa katika mwendo kasi.
Kufuatia taarifa hiyo, mpelelezi Dotto aliungana na timu ya askari wengine na kuelekea eneo la tukio Kiwalani ambapo waliu
mkuta mwanaume huyo akigugumia kwa maumivu makali na hawezi kuongea.
Polisi walimpeleka mtu huyo ambaye alikuja kujulikana kuwa ni Ally, katika Hospitali ya Amana kabla ya kupewa rufaa na kumhamishia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alifariki muda mfupi baadaye.
Bodaboda mwerevu
Vidokezo vya nini hasa kilimpata Ally vilianza kuonekana usiku wa Novemba 11, 2013 wakati mwendesha bodaboda katika mji wa Chalinze, mkoani Pwani, Rajabu Hassan Khalfan, alipokuwa katika shughuli zake za kawaida.
Wakati akisaka abiria pembezoni mwa barabara kuu ya Chalinze-Arusha, umbali wa kama kilomita moja kutoka katikati ya mji wa Chalinze, aliona gari likiwa imeegeshwa kandokando ya barabara na mmoja kati ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo akimwashiria kusimama.
Rajabu alitii wito na kusimama. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu sita na mtu aliyemwashiria kusimama alimwomba aende kuwatafutia fundi makenika awasaidie kutengeneza gari lao alilodai lilikuwa limeharibika. Rajabu alikubali na kubadilishana namba za simu.
Wakati Rajabu akirandaranda kutafuta fundi, mtu yule aliyemwomba awatafutie fundi wa gari alimwita tena. Zamu hii anamwomba amtafutie pia mnunuzi wa gari chakavu endapo atakosa fundi.
Kufuatia ombi hilo la pili, bodaboda aliingiwa na shaka kuwa kulikuwa na jambo si la kawaida kuhusu watu wale. Alipotoka pale alikwenda moja kwa moja katika Kituo cha Polisi Chalinze na kuripoti suala hilo.
Alipofika kituoni alikutana na Inspekta Msaidizi wa Polisi aliyejulikana kwa jina la Uledi akamweleza wasiwasi wake juu wa watu wale. Hapo, Uledi alimwomba mwendesha bodaboda ampeleke eneo la tukio huku yeye (Uledi) akijifanya ndiye mnunuzi wa magari chakavu.
Walipofika waliwakuta watu wawili tu wamesalia ndani ya gari hilo huku wanne wengine wasijulikane walipo. Waliokuwa ndani ya gari ni Msafiri Emmanuel Daniel ambaye rufaa yake imetupwa hivi karibuni na Jailos Aidan ambaye alifariki dunia wiki chache kabla ya kusikilizwa rufaa yao.
Gari hilo lilikuwa na namba za usajili za IT 1340 zikiashiria kuwa lilikuwa likisafirishwa kwenda nchi jirani. Hata hivyo, upekuzi zaidi wa polisi uligundua kulikuwa na namba nyingine za gari T864 AHQ zilizokuwa zimefichwa ndani ya gari hilo.
Baadaye iligundulika kuwa namba hizo zilifanana kabisa na namba za gari lililoporwa kutoka kwa marehemu Ally.
Polisi waliwakamatwa watuhumiwa hao kwa kushukiwa kutumia gari linalosadikiwa kuwa la wizi. Wakati wakiendelea na upelelezi, askari wa Chalinze walipokea taarifa kuwa gari walilolikamata lilikuwa likitafutwa jijini Dar es Salaam kuhusiana na tuko la mauaji.
Kufuatia taarifa za kupatikana kwa gari hilo Chalinze, askari wawili wa upelelezi kutoka Dar es Salaam, Koplo Mselemu and Koplo Ismail wakiongozana na baba wa marehemu Ally, Hemed, walisafiri hadi Kituo cha Polisi Chalinze.
Katika Kituo cha Chalinze, Mzee Hemed alilitambua gari hilo kuwa ndilo alilomkabidhi mwanae alitumie kwa biashara ya teksi. Watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa askari wa Dar es Salaam na kuondoka nao wakiongozana na Mzee Hemed.
Hiyo ilikuwa ni Novemba 12, 2013, siku tatu tu baada ya kuporwa kwa gari hilo na kuuawa kwa Ally.
Baada ya kesi yao kusikilizwa, Mahakama Kuu iliwatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa.
Rufaa yasikilizwa
Mwaka 2018, Msafiri na Jailos walikata rufaa katika Mahakama ya Rufani Dar es Salaam wakipinga kutiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa.
Wakili aliyekuwa akimtetea Msafiri, Merkior Sanga aliomba mahakama imwachie huru, akidai kuwa taarifa ya onyo ambayo mrufani alirekodi na polisi ambayo alidaiwa kukiri kufanya kosa ilichukuliwa nje ya muda wa kisheria.
Kifungu cha 51 (1) (a) au (b) ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inaelekeza kuwa maelezo ya onyo kutoka kwa mtuhumiwa yarekodiwe ndani ya saa nne tangu kukamatwa kwa mtuhumiwa isipokuwa tu pale ongezeko la muda linapoombwa na kukubaliwa na mahakama.
Sanga alidai kwa kuwa hakukuwa na kibali cha kuongeza muda wa kuchukua maelezo ya onyo, maelezo hayo ya mrufani yalipaswa kuondolewa kwenye orodha ya ushahidi kwa kuchukuliwa nje ya muda wa kisheria.
Polisi lawamani
Lakini katika hukumu yao ya hivi karibuni, majaji wa Mahakama ya Rufani Rehema Mkuye, Barke Sehel na Ignas Kitusi walikubaliana na wakili Sanga kuwa taarifa ya onyo kwa mtuhumiwa ilichukuwaliwa nje ya muda unaotakiwa kisheria.
Hata hivyo, majaji hao wametumia hukumu hiyo kueleza kushangazwa kwao na ukiukwaji mkunbwa wa taratibu za kisheria zinazolinda haki za watuhumiwa.
“Kwa hiyo tunakubaliana na wakili Sanga kuwa maelezo ya onyo yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria na hatukubaliani na Leopold (wakili mwandamizi wa serikali) kwamba uchunguzi wa kesi hiyo ulikuwa mgumu kiasi cha kuhalalisha ucheleweshwaji huo,” walisema majaji hao.
Wakaendelea: “Tunadhani fursa imejileta yenyewe kwa sisi kusisitiza msimamo wetu wa kudumu kuhusu kutotimiza takwa la kifungu cha 50 na 51 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Ni wazi kuwa katika kesi hii na nyingine nyingi polisi hawakulipa umakini unaotakiwa suala la kuchukua maelezo ya onyo.”
Hata hivyo, majaji hao walitupilia mbali rufaa ya Msafiri baada ya kukubaliana kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa ndiye aliyekamatwa Chalinze akiwa na gari ambalo Ally alikuwa akiliendesha kabla kukutwa na mauti.