Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amempongeza Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, kwa kutambua kwamba Tanzania haina Corona na ndiyo maana hakuvaa barakoa, ambapo alimshika mkono na kwenda kula wote chakula.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 8, 2021, wakati akizungumza mara baada ya serikali kupitia Shirika la Reli la Tanzania TRC, kusaini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Mwanza hadi Isaka na moja ya kampuni kutoka nchini China, ambayo ilishinda zabuni katika ujenzi huo.
"Ninampongeza sana Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, anajua Tanzania hatuna Corona, ndiyo maana hakuvaa hata yale mabarakoa na mimi kwa kumthibitishia nakwenda kumshika mkono twende tukale chakula pamoja", amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema kuwa, "Tumeeleza hali halisi kwamba China ni nchi tajiri Duniani na sisi Tanzania tuna mazao mengi tunayoweza kuyapeleka China na ndiyo maana katika zawadi zangu nimetoa korosho, majani ya chai na Kahawa, nikiamini kuwa wachina wakila tu nusu kilo ya korosho zetu, maana yake watakuwa wanakula Tani milioni 750 na korosho zote za Tanzania zitakuwa zimeisha".