Waziri wa Mambo ya nje Dkt. Palamagamba Kabudi awapa neno wale wote wasiotakia mema na waliokuwa wanabeza mabadiliko ya sheria katika sekta ya madini kwamba yatafukuza wawekezaji.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba kati ya serikali na Lz Nickel Limited mkoani Kagera , Kabudi amempongeza Rais wa Jamhuri wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa ujasiri na msiamamo wake thabiti.
"Wale wasiotutakia mema walitutisha kwamba sasa tumefukuza wawekezaji wa madini nchini Tanzania, na kwa kweli bila ujasiri wako na msimamo wako thabiti tungeyumba, lakini leo namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwamba amefanya wale wote waliotu zoza kwamba sheria hizi na msimamo huu utatufukuzia wawekezaji, leo tumepokea wawekezaji wakubwa katika madini adimu duniani" amesema Kabudi.
Aidha Dkt.Kabudi amesema kuwa sheria hizo kwenye madini zimeleta mageuzi na sura mpya katika umiliki, ulinzi, usimamiaji, utawala na matumizi ya utajiri na rasilimali asilia za nchi na umeleta mwanga wa matumaini kwa mchango na faidi zinazotarajia kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.