UPO uwezekano mkubwa wa kiungo mshambuliaji raia wa Kenya, Francis Kahata kuendelea kubaki Simba, huku Mghana, Bernard Morrison akitajwa kutemwa ili kumpisha profesheno mmoja.
Wakati Simba wakipanga kusitisha mkataba wa Morrison, inaelezwa kuwa, mabosi wa timu hiyo wamepata ugumu wa gharama kubwa za kuvunja mkataba ambazo ni Sh 250Mil.
Simba imepanga kuachana na Morrison ili kiungo mpya raia wa Zimbabwe, Perfect Chikwende achukue nafasi yake.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, mabosi wa Simba wanafikiria kumuacha Morrison ambaye anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita kutokana na kuugua.
Aliongeza kuwa mabosi hao wameona ni bora wakabaki na Kahata ambaye hana majeraha yoyote watakayemtumia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
“Kama uongozi tumeingia hofu ya wachezaji wetu waliokuwepo katika michuano ya CHAN, kwani mara kadhaa wachezaji wanapotoka katika michuano hiyo kunakuwepo na majeruhi katika timu.“
Hivyo basi kwa tahadhari tumeona ni bora tumbakishe kwanza Kahata kwa hofu ya kutokea majeruhi mara wachezaji wetu watakaporejea, pia wale wapya tuliokuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wao ambao nao wapo Cameroon wakicheza Chan akiwemo Karim (Ntikubuka).
“Ni bora tukaachana na Morrison ambaye ni mgonjwa na kumbakisha Kahata asiye na majeraha yoyote na ni msaada katika timu, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kubakia Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Hivi karibuni alisikika mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Kassim Dewji ‘KD’ akizungumzia ishu ya ugonjwa anaoumwa Morrison, alisema: “Morrison ni mgonjwa ana tatizo la hernia ambalo huenda likamuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita kwa ajili ya matibabu.”
WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA, Dar