UONGOZI wa Simba, umeweka wazi kuwa hakuna sababu ya kushindwa kuwafunga Platinum FC kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utachezwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu kwenye ukumbi wa mkutano uliopo Serena Hotel Dar, Msemaji wa Simba Haji Manara, alisema wana historia kubwa kwenye mashindano hayo na kwamba timu kubwa kama As Vita, Al Ahly, JS Soura na timu zingine zilifungwa kwa Mkapa itakuwaje washindwe kuwafunga Platinum.
Manara alisema maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo yapo tayari kwa asilimia 100 na jana timu hiyo ilipasha misuli moto kwenye Uwanja wa Mkapa na leo Jumanne watakuwa kwenye uwanja wao wa Mo Simba Arena kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.“
Ombi letu tulilopeleka Shirikisho la Soka Afrika (Caf ), la mchezo kurudishwa nyuma kutoka saa 1:00 usiku hadi saa 11:00, limekubaliwa.
Kwa hiyo mchezo upo palepale na utapigwa saa 11:00 za jioni pale kwa Mkapa. Tuliomba muda irudishwe nyuma kutokana na miundombinu ya mji wetu tunataka watu waje na wawahi kurudi makwao.
“Nitumie nafasi hii kuwaambia Wanasimba wote na Watanzania, Simba tunakwenda kuweka rekodi ya kufuzu kucheza hatua ya makundi kwa mara ya pili kwenye nchi hii, hakuna timu nyingine yoyote ya Tanzania tangu dunia hii iumbwe sisi ndiyo tunakwenda kuwa wa kwanza.
“Kama Nkana, As Vita, Al Ahly, Js Soura na hao wengine walikufa hapa Dar es Salaam, hao Platinum ni akina nani. Hawatoki kivyovyote vile, lazima waondoke, lakini hii itachagizwa vikubwa na uwepo wa mashabiki na sapoti ya Watanzania wote.
“Punguzo la tiketi kutoka shilingi 7,000 hadi 5,000 kwa mzunguko kama ambavyo tulitangaza, inatarajiwa kumalizika 5:59 usiku wa leo (jana), wakati zile za V.I.P A na B ambavyo ni shilingi 40,000 na 100,000, zitabaki kama zilivyo.
Lakini leo (jana), gari la matangazo litakuwa linapita mtaani kuuza tiketi,” alisema Manara.HII NDIYO MAANA HALISI YA WAR IN DARManara pia aliweka bayana kuwa kauli mbiu ya War In Dar, ilikuja wakiwa wanalenga kuhamasisha ushindi kwenye mchezo huo kufa na kupona, lakini haikuwa na maana yoyote ya uvunjifu wa amani.“
Ile War In Dar ilikuwa na maana ya kuhamasisha kupigana kufa na kupona ndani ya uwanja dakika 90 kusaka ushindi. Siyo vurugu wala vita ya mabunduki, vita ni pale wanaume 22 watakapokwatuana uwanjani.“
Kwetu sisi huu mchezo una umuhimu zaidi ya watu wengine wanavyofikiria, tunataka historia na rekodi mpya kwenye nchi hii, narudia kusema tunataka kwenda hatua ya makundi kwa mara nyingine tena. Mashabiki wakiimba War In Dar kwa dakika zote 90, wale Platinum wanatokaje, alikufa Mwarabu hapa,” alisema.
UWANJA KUJAA ASILIMIA 100
Manara alitoboa siri kuwa wamepeleka ombi lingine Caf la kuomba mchezo huo uhudhuriwe na mashabiki kwa asilimia 100 kwa maana uwanja wote ujae kama kawaida na siyo asilimia 50 kama ambavyo Caf wameelekeza.“Tuendelee kuomba Mungu ombi letu la kuujaza Uwanja wa Mkapa kwa asilimia 100 likubaliwe, tumeshapeleka ombi Caf, nafikiri muda siyo mrefu tutapata mrejesho na ndiyo maana tunasisitiza mashabiki waendelee.
GPL