Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewaagiza Watanzania kutumia mvua zinazonyesha kipindi hiki kulima mazao ya chakula na biashara ili kuepukana na janga la njaa, na endapo eneo lolote litakumbwa na njaa serikali haitokuwa tayari kupeleka chakula.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo akiwa Wilayani Bahi mkoani Dodoma wakati akielekea jijini humo akitokea Tabora, amesema kuwa maeneo ambayo hayatafanya kazi kwa uzembe wao hatovumilia viongozi wa maeneo husika.
“Sitatoa chakula kwenye Wilaya yoyote, hakuna chakula cha bure kama mlivyozoea huko nyuma, usipofanya kazi usile na usipokula kufa, lazima tuambiane ukweli, Watu wafanye kazi, walime, na asiyefanya kazi asile”, amesema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa, “Wilaya itakayopata njaa DC ataondoka na Viongozi wengine wanaostahili kuhamasisha Wananchi kufanya kazi wataondoka, tunataka pesa tunayopata ifanye kazi nyingine, tunatoa Elimu bure, tunajenga SGR ndio kazi za Serikali, sio kukulisha".