Kesi ya Rais wa zamani wa Marekani itaanza wiki ya pili ya Februari katika Bunge la Seneti, baada ya kuwasilishwa mashitaka katika taasisi hiyo mapema wiki ijayo, maafisa wa chama cha Democratic katika Baraza la Congress wamesema.
“Mara baada ya faili hizo kutayarishwa, kesi itaanza wiki ya Februari 8,” amesema Chuck Schumer, kiongozi wa chama cha Democratic katika Bunge la Seneti, ambapo Donald Trump atasikilizwa kwa madai ya “kuchochea uasi”.
Chuck Schumer hapo awali alikuwa amewaambia wenzake kwamba mashtaka “yatapelekwa katika Bunge la Seneti Jumatatu”.
Kufikia sasa, Joe Biden amejizuia kuingilia kati suala hili, akibaini kwamba ni kwa Bunge la Seneti lenyewe kuweka masharti ya kesi ya mtangulizi wake.
Donald Trump anatuhumiwa kuwa aliwahimiza wafuasi wake kuanzisha shambulio katika majengo ya Bunge la Seneti, Capitol Hill, Januari 6, wakati wawakilishi wabunge na maseneti walikuwa wakiidhinisha ushindi wa Joe Biden aliyetangazwa kushinda uchaguzi wa urais.