Kiongozi wa Korea Kaskazini KimMaelezo Jong-un amekubalia kuwa mpango wake wa kiuchumi wa miaka mitano kwa nchi hiyo ambayo imejitenga, ulishindwa kufikia malengo yaliyowekwa "katika karibu kila sekta".
Korea Kaskazini ilifunga mipake yake Januari mwaka jana kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona licha ya madai kwamba hakujawahi kuwa na maambukizi ya virusi hivyo nchini humo.
Hatua hiyo imesababisha kujitenga na majirani zake ambayo pia ni washirika wake wa karibu China.
Biashara kati ya nchi hizo mbili imedorora kwa asilimia 80. Aidha, kimbunga na mafuriko pia vimesababisha nyumba na mazao kuharibika huko Korea Kaskazini ambayo bado imewekewa vikwazo vikali vya kimataifa ikiwemo juu ya mpango wake wa nyuklia.
Sio jambo la kawaida kwa Bwana Kim kukubali makosa yake - hatua ambayo imekuwa kama utambulisho wake amesema Laura Bicker mwandishi wa BBC mjini Seoul.
Taarifa kupitia televisheni imeonesha wakiwa kwenye mkutano katika mji mkuu wa Pyongyang, uliokuwa umejaa maelfu ya wanachama na hakuna ambaye alikuwa amevaa barakoa walipokuwa wamesimama kupiga makofi wakimkaribisha Bwana Kim wakati anaingia.
Katika hotuba yake, Bwana Kim alisema mkakati wake wa miaka mitano alioutangaza mwaka 2016 "umekosa kufanikiwa kwa karibu kila sekta" na ni lazima mtu akubali kuwa alikosa.
Alitoa wito wa kujitegemea na kusifu wanachama kwa kukabiliana na tishio la janga la virusi vya corona.
Korea Kaskazini ilisema kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa maelfu ya watu wanashukiwa kupata maambukizi lakini haijawahi kukubali kuwa imethibitisha kisa chochote cha maambukizi ya virusi vya corona.
Hata hivyo, bado haijafahamika itakabiliana vipi na moja kati ya miaka ambayo imekuwa changamoto zaidi kwa nchi hiyo katika kipindi cha miongo kadhaa, mwandishi wa BBC amesema.
Bwana Kim anatarajiwa kutangaza mpango mpya wa miaka mitano katika mkutano huo.
Hotuba yake inawadia wiki mbili tu kabla ya Rais mteule wa Marekani Joe Biden kuchukua madaraka na Donald Trump kuondoka ambaye wamekuwa na uhusiano mzuri naye hata ikiwa ni hatua ndogo iliyopigwa ya majadiliano juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.