BAADA ya Uongozi wa Gwambina FC kuachana na benchi la ufundi la timu hiyo lililokuwa linaongozwa na Kocha Mkuu, Fulgence Novatus na msaidizi wake Athuman Bilal inaelezwa kuwa aliyekuwa kocha msaidizi ndani ya Klabu ya Simba, Masoud Djuma ametuma CV kuomba kazi.
Tangu Januari 4 benchi hilo la ufundi lilifutwa kazi na kwa sasa timu ipo chini ya Khassain Salum pamoja na Seleman Kisedi sababu ilielezwa kuwa ni mwendo mbovu wa timu hiyo ambayo ipo nafasi ya 14 na pointi 19 baada ya kucheza mechi 17.
Taarifa kutoka ndani ya Gwambina zimeeleza kuwa kuna maombi ya makocha wengi wa Bongo na nje ya Bongo ikiwa ni pamoja na Djuma aliyeifundisha Simba msimu wa 2017/18.
“Makocha wengi wametuma CV kuomba kazi ya kuinoa Gwambina ambayo kwa sasa haina kocha, lipo jina la Djuma,(Masoud) pia kocha wa Biashara United, Francis Baraza naye pia pamoja na wengine kutoka Burundi,” ilieleza taarifa hiyo.
Mohamed Almas, Mkuu wa Idara ya Mashindano ndani ya Gwambina FC amesema kuwa ni kweli kuna maombi mengi ndani ya timu hiyo mchakato ukikamilika kila kitu kitawekwa wazi.
“Kuna majina ya makocha wengi wenye uzoefu, tunahitaji kumpata kocha mapema kabla ya ligi kurejea hivyo hivi karibuni atajulikana mrithi mashabiki wasiwe na mashaka,” amesema.