Dar es Salaam. Si rahisi kuamini lakini ndivyo ilivyokuwa kwamba maisha ya aliyekuwa mwanasheria mahiri wa Katiba, mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, yalikatishwa wakati majambazi wakiiba Sh2 milioni, kompyuta mpakato moja na simu zake nne za mkononi.
Kifo cha Dk Mvungi, siku tisa baada ya kushambuliwa na kuumizwa vibaya, kililishtua Taifa huku wengi wakishindwa kuamini kama kweli uhai wa mtu aliyetoa maisha yake kwa watu na nchi yake unaweza kupotea kwa wizi wa mali ndogo kiasi kile.
Kukamatwa kwa watuhumiwa na baadaye kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kumesaidia haki kutendeka, lakini hukumu hiyo kamwe haitaweza kufidia hasara ya kumpoteza nguli huyo wa sheria.
Miaka saba baada ya kifo chake, maswali kuhusu nini hasa ilikuwa nia ya wavamizi wake yameendelea kuumiza vichwa vya wengi.
Ni usiku wa Novemba 3 mwaka 2013. Dk Mvungi akiwa amepumzika na mke wake, Anna nyumbani kwao Kibwegere Msakuzi, Kata ya Mbezi, ghafla wanasikia mshindo wa risasi.
Wakiwa wanajiuliza kinachoendelea, kundi la watu sita lilivamia ,wakaingia ndani ya nyumba yake baada ya kuvunja mlango wa jikoni. Mke wake alipiga mayowe ya kuomba msaada bila mafanikio.
Alipoamua kutoka chumbani na kufuatilia alikutana na wahalifu koridoni wakiwa wameshika mapanga. Wavamizi wale walimwamuru awape pesa. Hakubisha. Alikwenda moja kwa moja chumbani kwake na kutoka na bahasha iliyokuwa na Sh2 milioni na kuwapa.
Baada ya kuwakabidhi pesa hizo wakamweka chini ya ulinzi na kumwamuru alale chini huku wakiendelea kupekua chumbani kwake na sehemu nyingine za nyumba.
Watu hao walifanikiwa kupata bastola iliyokuwa imehifadhiwa katika droo ya kitanda cha Dk Mvungi. Bastola ile ilikuwa mali ya Hellen Eshers, ambaye alikuwa mteja wa Dk Mvungi katika masuala ya kisheria.
Wakati huo Eshers alikuwa amefariki na bastola ile ilikuwa imehifadhiwa kwa Dk Mvungi ikisubiri shauri la mirathi ya mama huyo ambalo alikuwa akilisimamia.
Mbali na pesa na bastola, wavamizi hao walichukua kompyuta mpakato na simu nne za mkononi.
Mvungi aumizwa
Baada ya wahalifu hao kutokomea, mke wa Dk Mvungi aliamka na kuanza kumtafuta mumewe. Alimkuta jikoni akiwa amekaa chini na hajitambui. Alikuwa akivuja damu nyingi huku akiwa na jeraha kubwa kichwani na uso wake ukiwa umevimba.
Bila kupoteza muda familia ilianza jitihada za kumpeleka hospitali. Kwanza walimpeleka Hospitali ya Tumbi Kibaha ambako, jeraha kubwa kichwani lilishonwa kabla ya kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akiwa Muhimbili, Dk Mvungi alipelekwa moja kwa moja chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako alitibiwa kwa siku tatu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini, kwa matibabu zaidi.
Dk Mvungi pic 2
Watuhumiwa sita wanaodaiwa kumuua aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wakiwa chini ya ulinzi wakati wakitoka chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi alisindikizwa na mmoja wa mwanafamilia yake, Deo Mwarabu.
Habari za kushambuliwa kwa Dk Mvungi zilitawala vyombo vya habari huku polisi wakiwa wamenzisha msako mkali kuwatafuta wauaji hao. Shinikizo la umma kutaka haki itendeke liliongezeka siku hadi siku.
Dk Mvungi afariki
Siku saba baadaye Taifa lilipokea taarifa ya kufariki kwa Dk Mvungi akiwa anatibiwa Afrika Kusini. Viongozi waandamizi serikalini, wanasheria na makundi mbali mbali ya kijamii na wananchi wa kawaida walituma salamu za pole wakieleza kusikitishwa kwao na kifo cha mwanasheria huyo nguli.
Mwili wake uliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Novemba 16, mwaka 2013, saa 1:05 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege Afrika Kusini.
Mke wake Anna, watoto na wanafamilia ambao walikuwa wamevalia suti nyeusi walikuwepo JNIA kuupokea mwili wa mpendwa wao. Vilio na majonzi vilitawala baada ya mwili kutua JNIA na kupokelewa.
Viongozi wa kitaifa walifika uwanjani hapo kuupokea mwili wa Dk Mvungi akiwamo aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi (Sasa Rais wa Zanzibar) na aliyekuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki.
Pia, wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na mwenyekiti wao, Jaji Joseph Warioba pamonj na mwenyekiti mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba walikuwapo.
Siku iliyofuata (Novemba 16, 2013) mwili wa Dk Mvungi uliagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambako wanasheria, viongozi wa Serikali, walimu na wanafunzi wa vyuo na wengine wengi walijitokeza.
Baada ya kuaga, mwili wake ulisafirishwa kwenda wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwa mazishi.
Azikwa kijijini kwao
Dk Mvungi alizikwa Novemba 19 mwaka 2013 kijijini kwao, Chanjale, Kisangara Juu katika mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi wengi wa kanisa na Serikali.
Wakati Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda akiongoza viongozi wa Serikali katika mazishi hayo, Askofu Rogath Kimaro wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Same aliongoza viongozi wa kiroho.
Askofu haamini ujambazi
Akizungumza katika misa ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Kisangara Juu, Askofu Kimario alisema kushambuliwa kwa mwanasiasa huyo halikuwa tukio la ujambazi.
Alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa kimtandao na kuitaka Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo badala ya majibu mepesi yasiyofanyiwa utafiti.
“Eti waliotenda hilo ni majambazi, nani kasema ni majambazi?... Ni research (utafiti) ipi ama upelelezi gani umefanyika? Hawa ni wauaji wa kimtandao, kuna maswali mengi yasiyo na majibu,” alisema Askofu Kimario.
Kauli hiyo ilionekana kujibu aliyoitoa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa mauaji ya Dk Mvungi ni ujambazi.
Askofu Kimario alisema Watanzania wanamlilia Dk Mvungi na familia yake inamlilia kama wasomi na wanazuoni wanavyomlilia hivyo Serikali inawajibika kutoa majibu sahihi juu ya kifo chake.
“Damu yake inadai Watanzania tujiulize Dk Mvungi yuko wapi... wanausalama ndugu yetu yupo wapi? Wasomi mlikuja hapa kwenye harusi yake mkafurahi naye leo mnatuletea marehemu,” alisema.
Askofu huyo alisema kinachofanya Taifa kubwa kama Marekani liheshimike ni wepesi wake wa kuwaeleza wananchi wake ukweli na kutaka Watanzania wasiridhike na majibu mepesi ya kifo hicho.
Misa hiyo ilihudhuriwa pia na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus Kinyaiya na Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa Katoliki.
Akitoa salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inafanya jitihada kuwakamata waliohusika na mauaji ya Dk Mvungi.
“Ni kweli Serikali inafanya jitihada za kuwakamata waliofanya tukio hili la ovyo lakini hata tukiwapeleka mahakamani wakahukumiwa kunyongwa hiyo si mbadala wa Dk Mvungi,” alisema Waziri Pinda.
Jaji Warioba, aliyefanya kazi na Dk Mvungi kwa muda wa kukusanya maoni juu ya mabadiliko ya Katiba alisema watamuenzi Dk Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi makubwa kwa nchi ili mchango wake uendelee kuishi miaka mingi ijayo.
Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kifo cha Dk Mvungi kimewaumiza lakini akasisitiza hawatarudisha nyuma harakati za kupigania haki za Watanzania.
Itaendelea kesho