Kuapishwa Biden: Watu kadhaa wajitokeza kuandamana Marekani



Vikundi vidogo vya waandamanaji - baadhi yao wakiwa na silaha - wamekusanyika nje ya majengo ya serikali ya Marekani, ambapo kuna mvutano mkubwa baada ya jengo la Capitol Hill kuvamiwa huko Washington.

Maandamano yanafanyika katika majimbo ya Texas, Oregon, Michigan, Ohio na kwingineko.


Lakini kulikuwa na hali ya utulivu Jumapili, baada ya kuimarishwa kwa ulinzi katika bunge congress la Marekani.


FBI imeonya juu ya maandamano yenye silaha kabla ya kuapishwa kwa Biden siku ya Jumatano.


Rais mteule Joe Biden atachukua madaraka wiki mbili baada ya waandamanaji wafuasi wa Bw Trump kushambulia Jengo la Capitol la Washington mnamo Januari 6, na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo afisa wa polisi.


Miji mingi imejiandaa kwa maandamano yanayoweza kuwa na vurugu mwishoni mwa wiki, huku vikosi vya usalama vikiwa vimeimarisha ulinzi.


Machapisho ya kwenye mitandao yanayomuunga mkono Trump na yaliitisha maandamano yenye silaha siku ya Jumapili, lakini wanamgambo wengine waliwaambia wafuasi wao wasihudhurie, wakidai ni jambo lililopangwa na askari kama mtego.


Kufikia sasa, ni idadi ya watu wachache tu ndio wamekusanyika katika baadhi ya miji , na kuacha barabara zinazozunguka majengo mengi ya serikali kuwa hazina watu.


Jarida la New York Times liliripoti kuwa zaidi ya washiriki 20 wa vuguvugu la Boogaloo Bois walikuwa miongoni mwa waandamanaji wenye silaha ambao walikusanyika katika jengo la serikali huko Columbus, Ohio.


Lakini wanaume ambao ni wanachama wa kundi lenye msimamo mkali ambalo linataka kuipindua serikali ya Marekani - wanasema walipanga kwa muda mrefu kuwa na maandamano ya silaha.


Wakati huohuo huko Michigan, watu zaidi ya ishirini wakiwa wamebeba bunduki - waliandamana nje ya jengo la serikali huko Lansing, huku polisi wakiwatazama tu.


"Sikuja hapa kufanya vurugu na natumani hakuna mtu atakayejitokeza kuwa mkali," mwandamanaji mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters.


Kundi lingine dogo la waandamanaji kama kumi hivi wakiwa na bunduki, walisimama nje ya Jumba la Texas huko Austin.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad