“UKIFIKA hotelini, kama huna fedha, utaishia kununua maandazi.” Joackim Mwakalobo, mkazi wa Mbalizi mkoani Mbeya, analalamika kuhusu gharama kubwa za chakula kwenye hoteli zilizoko barabara kuu ya Tanzania-Zambia.
Mwakalobo anawasilisha malalamiko yake katika hali ya simanzi akisema: “Unawekewa chipsi kavu Sh. 3,000 na zinakuwa kidogo sana, tena za baridi na unaambiwa ulipie na cha kubebea Sh. 500.
“Hii ni kero kubwa kwetu sisi abiria wa mabasi ambao wengi wetu vipato vyetu ni vya kundunduliza. Mbaya zaidi, usiponunua kwenye hoteli yanakosimama mabasi, huna tena pengine pa kununua chakula.
“Ninafikiri kuna haja serikali kuweka bei elekezi kwenye hizi hoteli yanakosimama mabasi, ili kutatua tatizo hili linalochochewa na madereva ambao hotelini wanakula bure na wanapewa posho kwa kupeleka abiria kwenye hoteli husika.”
Elina Kiwele, mkazi wa Dodoma, anaungana na Mwakalobo, akisema pamoja na vyakula kuuzwa kwa bei ghali, mazingira ya baadhi ya hoteli na migahawa yanakosimama mabasi, hayako katika viwango vinavyokubalika.
“Ukiingia chooni hata hamu kula inaondoka kutokana na uchafu uliokithiri huko,” anasema Kiwele.
KAULI YA TAKUKURU
Huku kukiwa na malalamiko hayo yanayotoa ishara ya kuwapo viasharia vya rushwa na uonevu dhidi ya abiria, Nipashe inatua mezani kwa Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Makao Makuu, Doreen Kapwani, kusaka majibu ya kinacholalamikiwa.
Katika majibu yake kwa gazeti hili, Kapwani anakiri taasisi hiyo kuwa katika uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili madereva wa mabasi na wamiliki wa hoteli na migahawa ya barabarani yanakopita mabasi ili abiria wake wapate huduma ya chakula na choo, maarufu ‘kuchimba dawa’.
“Suala hilo tunalo tunalifanyia kazi. Tunaangalia kama huo utaratibu na makubaliano ya wenye hoteli na madereva wa mabasi yana viashiria vya rushwa,” anasema.