Chato. Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania yenye namba T5H-TCD imeshusha abiria kwa mara ya kwanza katika uwanja wa ndege Geita - Chato wakitokea jijini Dar es Salaam.
Ndege hiyo imepokelewa na baadhi ya mawaziri, akiwemo Waziri Ujenzi na Uchukuzi Dk Leornad Chamuriho, Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Gabriel, wafanyabiashara pamoja na wananchi wa wilaya ya Chato.
Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa safari za ndege Chato, Dk Chamriho amesema kutua kwa ndege hiyo ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya kuhakikisha maeneo yote yanafikika kwa urahisi ili wananchi wafaidike na mnyororo wa thamani wa bidhaa zao.
Mbunge wa jimbo la Chato, Dk Merdad Kalemani amesema wakazi wa Chato watatumia uwanja huo kama fursa katika shughuli za kiuchumi.
Amesema wilaya ya Chato na Geita inautajiri wa madini, samaki na ardhi yenye rutuba hivyo ni fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika wilaya hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema mkoa huo utaunganisha Geita na Dunia nzima hivyo ni fursa kwa wakazi wa Geita kuchangamkia fursa za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni, hotel na kufungua makampuni ya usafiri kwa ajili ya kupeleka abiria katika uwanja huo.