KUNDI la watu zaidi ya 40 Wavamia Masista na Kuiba Fedha Milioni 16



KUNDI la watu zaidi ya 40 wanaodaiwa kuwa watumishi wa kampuni moja ya udalali wamevamia makazi ya watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Franciscan na kuchukua fedha zaidi ya Sh milioni 16.

Aidha watu hao ambao pia walivamia kituo cha malezi ya vijana wameharibu vifaa na samani zenye thamani ya Sh milioni sita.


Imedaiwa kuwa watu hao walikuwa wamebeba nondo walizotumia kuvunja makufuli ya lango kuu la kuingia kwenye makazi hayo na mengine ya ndani.

Tukio hilo lililotokea Januari 13, mwaka huu saa 7:45 mchana kwenye makazi hayo yaliyopo mtaa wa Engosingiu, kata ya Sinoni, jijini Arusha na kutolewa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Muriet iliyosajiliwa namba MTR/RB/186/2021.

Uvamizi huo ulizua taharuki kwa masista hao pamoja na majirani kutokana na namna watu hao walivyokuwa wakitumia nguvu kuvunja makufuli ya milango kwa kutumia nondo na majembe kisha kutoa vitu nje.


Akizungumza na waandishi wa habari, Sista Kiongozi, Meseret Melese alisema fedha zilizoibwa zilikuwa zimetolewa benki kwa ajili ya kwenda kutekeleza shughuli za shirika hilo kwenye mikoa mbalimbali ambapo kutokana na tukio hilo imewalazimu kufuta safari zote.

Alisema watu hao pia waliiba kompyuta mpakato moja, kuharibu kompyuta ya mezani, friji na kuvunja samani mbalimbali wakati walipotumia nguvu kurusha nje vitu hivyo.


Alisema makao hayo ya masista na malezi ya vijana na kazi za kichungaji yanatumiwa na masista 10 pamoja na vijana nane wanaoandaliwa kuwa masista, ambapo wakati watu hao wakivamia walikuwa masista sita na vijana nane.

Sista Mesele alisema siku ya tukio akiwa ndani alisikia kelele na alipotoka nje mlinzi wa getini alimfuata akiwa anakimbia na kumwambia kuna watu wengi wanalazimisha kuingia ndani.


Alisema kabla hajamaliza kumweleza tayari watu hao walikuwa wameshafika alipokuwa na kuingia ndani ambapo alijaribu kuzungumza nao hawakumsikiliza.

Alisema mtu mmoja alimwambia kuwa wamekwenda wenye eneo hilo kwani siku 14 walizopaswa masista hao kuwa wameondoka kama walivyoamriwa na mahakama zimekwisha.


"Niliwaambia tayari tumeweka zuio mahakamani kwani eneo letu halijaainishwa kwenye amri ya mahakama waliyotuletea hawakutaka kunisikia walikimbia wakaingia ndani wakaanza kubeba vitu wanatupa nje," alisema Sista Mesele.

Alisema watu hao baada ya kuona gari la polisi limefika walikimbia,

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salum Hamduni amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa mpaka sasa watu saba wanashikiliwa ingawa hakutaja majina yao.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi alikwenda kwenye makazi hayo ya masista ambapo aliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad