MWENYEKITI wa chama cha Civic United Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amemwomba aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kurejea tena katika chama hicho ili washirikiane kudai haki.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwakumbuka wanachama wa CUF waliopoteza maisha Januari 26 na 27 mwaka 2001 wakati wa maandamano ya amani, Lipumba aliwaomba wanachama wote waliohama CUF kurejea katika chama hicho ili kwa pamoja waweze kudai haki.
“Hata Maalim Seif karibu, unaweza kubaki ACT Wazalendo kulinda umakamu wa rais, lakini tunakukaribisha katika chama cha kudai haki. Wanachama wenzangu kwa sababu moja ama nyingine iwe kwa uongo uliozidishwa, rejeeni katika chama chetu kudai haki,” alisema Lipumba.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, aliondoka CUF Machi 2019 baada ya mgogoro wa uongozi kutokana na Lipumba ambaye alijiuzulu mwaka 2015 kurejea kwenye uongozi Julai 2016.
Mvutano huo wa uongozi ulihamia mahakamani lakini baada ya Lipumba kushinda kesi, Maalim Seif na kundi kubwa la wanachama wa CUF walihamia ACT-Wazalendo ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Baadhi ya viongozi waliotimka CUF na kumfuata Maalim Seif ni Joram Bashange, Nassoro Ahmed Marzui na Juma Haji Duni. Lipumba ametoa kauli hiyo ikiwa imepita miaka miwili ya malumbano baina yake na Maalim Seif.
Machi 2019, akizungumza katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CUF Buguruni, msomi huyo alimtaka Maalim Seif asiwaharibie chama chao.
Alisema Maalim anawafarakanisha watu waliokuwa pamoja, akidai ni mbinafsi na mtu hatari kwa kuwa aliwashawishi waliokuwa wabunge wa CUF kukihama chama hicho.
Machi 18, 2019 Lipumba alizungumza na Mwananchi na kueleza kuwa uamuzi wa kumfukuza Maalim Seif na wafuasi wake CUF ulikuwa ni wa kusikitisha lakini haukuwa na budi kwa sababu kiongozi huyo aliwasababishia matatizo.
Uamuzi wa Seif na timu yake ulikiathiri chama hicho, hasa Zanzibar ambako mbali na kupoteza maelfu ya wanachama, pia ofisi za chama hicho zilibadilishwa na kuwa za ACT Wazalendo.
Jana, msomi huyo hakurejea kauli hizo badala yake alisema huu ni wakati wa kujenga chama imara na kujenga mtandao mzuri wa chama kwa sababu chama imara ndicho kitakachosikilizwa kwamba madai yake ni ya msingi.
Kuhusu wanachama waliopoteza maisha mwaka 2001, Profesa Lipumba aliwataka wanachama kusamehe yote yaliyotokea lakini wasisahau.
Join Our Telegram Group for Job Updates CLICK HERE
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Magdalena Sakaya, alisema chama hicho kitaanzisha vuguvugu la kudai Katiba Mpya nchi nzima ili kupata Tume Huru itakayosimamia haki za wapiga kura.
“Hilo si jukumu letu CUF pekee yetu, tunaomba wananchi wote, taasisi mbalimbali tudai Katiba Mpya ili nchi yetu iwe na Tume Huru ya uchaguzi itakayosaidia kuondoa malalamiko baada ya uchaguzi,” alisema.