Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameondoa uwezekano wa nchi yake kuomba msamaha rasmi kwa dhuluma ilizozifanya nchini Algeria.
Ofisi yake imesema hayo jana kabla ya kutolewa kwa ripoti kuu kuhusu jinsi Ufaransa inavyokabiliana historia yake ya ukoloni.
Ofisi ya Macron imesema kuwa hakutakuwa na ''toba wala kuomba radhi" kwa kuikalia Algeria au vita vya umwagaji damu vya miaka minane ambavyo vilimaliza utawala wa Ufaransa na kuongeza kuwa kiongozi huyo wa Ufaransa badala yake atashiriki katika "matendo ya ishara" yanayolenga kuhimiza maridhiano.
Ufaransa iliikoloni Algeria kwa miaka mingi na hatimaye nchi hiyo mwaka 1962 ikapata uhuru baada ya miaka kadhaa ya mapambano ya ukombozi ya umwagaji damu.
Raia wa Algeria karibu laki tano waliaga dunia katika mapambano ya kuikomboa nchi yao.