Magufuli apigilia msumari wa mwisho kuhusu virusi vya corona



Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema baadhi ya Watanzania waliokwenda nje ya nchi kupata chanjo ya virusi vya corona wamerejea nchini baada ya kuchanjwa na “kutuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu.”


Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana wilayani Chato mkoani Geita katika hafla ya uzinduzi wa shamba la miti aliloita Silayo, lenye ukubwa wa hekta 69,000 ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini baada ya lile la Sao Hill lililopo wilaya ya Mafinga mkoani Iringa.


“Ninajua, wapo baadhi ya Watanzania hata wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walikochanjwa huko, wamekuja huku wametuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu,” alisema.


Rais Magufuli alieleza hayo, siku moja baada ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga kutoa waraka wa tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya corona ambavyo vimezishambulia nchi mbalimbali.


Pia, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango majuzi naye aliwataka watumishi katika wizara yake kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo licha ya kwamba ugonjwa huo haupo hapa nchini kwa sasa.


Taasisi mbalimbali za umma na ofisi za Serikali zimeanza kuchukua tahadhari kwa kurudisha utaratibu wa kuweka vitakasa mikono au maji tiririka na sabuni milangoni ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwenye ofisi hizo.


Wadau mbalimbali nchini wakiwemo wanasiasa wameanza kuendesha kampeni ya kuwataka Watanzania kuzingatia tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.


Hata hivyo, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kusimama imara dhidi ya vitisho wanavyovipata na kuwa waangalifu kwa mambo wanayoletewa kwa sababu yanaweza kuwaletea madhara makubwa kiafya.


“Ni lazima Watanzania tuwe waangalifu kwa mambo ya kuletewa letewa, msije mkafikiria mnapendwa sana. Taifa hili ni tajiri, Afrika ni tajiri, kila mmoja analitamani, tuwe waangalifu,” alisema Rais Magufuli huku akisisitiza kwamba “chanjo hazifai.”


Aliitaka wizara ya afya kutokimbilia masuala ya chanjo ya corona bila kujiridhisha kwa sababu siyo kila chanjo ina faida kwa Watanzania. Aliwataka Watanzania kuwa waangalifu wasije wakafanyiwa majaribio ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa.


“Naomba tuendelee kusimama na kumwomba Mungu wetu, tuendelee kumtanguliza Mungu wetu huku kukichukua tahadhari kadri tunavyoambiwa na wataalamu wetu,” alisisitiza Rais Magufuli.


Vilevile Rais Magufuli aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari za kiafya dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) ikiwa ni pamoja na kujifukiza na kumwomba Mungu.


Alisisitiza kwamba hatarajii kutangaza kuwafungia ndani Watanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine kwa sababu Mungu anawalinda. Hata hivyo, alisisitiza kwamba wataendelea kuchukua tahadhari nyingine za kiafya.


“Nchi nyingi wananchi wake watakuwa wamejifungia ndani, sisi Watanzania hatujajifungia ndani na wala sitegemei kutangaza hata siku moja kwamba tutajifungia ndani kwa sababu Mungu wetu yuko hai na ataendelea kutulinda Watanzania.


“Lakini pia tutaendelea kuchukua tahadhari zingine za kiafya ikiwa ni pamoja na kujifukizia. Unajifukizia huku unamwomba Mungu, unaswali, unasali huku unapiga zoezi la kufanya kazi, unalima mahindi, unalima viazi ili ule vizuri ushibe corona ishindwe kuingia kwenye mwili wako,” alisema Rais Magufuli.


Aliitaka wizara ya afya kuangalia afya za Watanzania bila kufanya papara ya kuingia kwenye majaribio ya chanjo ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya wananchi. Kiongozi huyo alisisitiza kwamba si kila chanjo ina faida.


Join Our Telegram Group for Job Updates CLICK HERE


“Tusije tukakimbilia kila kitu cha nje. Si kila kitu cha nje ni kizuri, si kila kitu tunacholetewa ni kizuri, hata kwenye mazao yetu, lazima tuhakikishe taasisi zetu za kitafiti zina-maintain (zinaendeleza) zile mbegu za asili ambazo ziko resistant (stahimilivu) kwenye mazingira yetu,” alisema kiongozi huyo.


Imeandikwa na Peter Elias, Aurea Simtowe, Elias Msuya na Rehema Matowo

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad